NEWS

Wednesday 23 June 2021

Mwenge wa Uhuru wazindua miradi ya maendeleo Tarime, kikiwemo kituo cha PKM




MWENGE wa Uhuru umewasili katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, ambapo umezindua miradi mbalimbali ikiwemo Shule ya Sekondari ya Murito na kituo kipya cha mafuta cha kampuni ya PKM kilichopo Gamasara, nje kidogo ya mji wa Tarime.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo hicho leo Juni 23, Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi amepongeza uwekezaji huo akisema una faida kwa wananchi na Taifa.

Luteni Mwambashi (katikati) na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kituo hicho.

“Kituo hiki kimesaidia kuboresha huduma ya mafuta, lakini pia uwepo wa sheli hii unasaidia kuongeza pato la Serikali, ambalo linasaidia miundombinu mbalimbali kwa Watanzania. Kwa hiyo tunakupongeza sana [mwekezaji PKM] kwa hatua kubwa uliyofikia.

“Lakini pia uwepo wa sheli hii umesaidia upatikanaji wa ajira kwa vijana 10, kwa hiyo imesaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, na kama tunavyofahamu hatuwezi kupata ajira wote serikalini. Nakupongeza sana kwa hilo,” amesema Luteni Mwambashi.



Kiongozi huyo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi wengine kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta mbalimbali ili kuchangia uboreshaji wa huduma, ajira na pato la Taifa.

Kwa upande mwingine, ametoa agizo kwa mwekezaji huyo kuwapa wafanyakazi mikataba ya ajira, ili kulinda haki za pande zote mbili (mwajiriwa na mwajiri).

Kampuni ya PKM imekuwa ya kwanza kujenga na kufungua vituo vya mafuta vya kisasa katika wilaya ya Tarime, ambavyo vimechangia kuboresha upatikanaji wa huduma ya mafuta, kubadilisha mji huo kuwa wa kisasa na kutoa ajira kwa vijana wa kike na kiume. Kampuni hiyo pia inamiliki na kuendesha hoteli ya kisasa ya PKM mjini Tarime.

Akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella wilayani Serengeti jana, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Salum Hapi amesema utakimbizwa kilomita 655 na kuzindua miradi mbalimbali 50 yenye thamani ya Sh bilioni 13.524 katika wilaya sita za mkoani Mara. Kesho mwenge huo utaendelea na mbio zake wilayani Rorya.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages