NEWS

Wednesday 23 June 2021

Mwenge wamulika ufisadi ujenzi bwalo la wanafunzi Serengeti, kiongozi wa mbio akataa kulizindua, aagiza TAKUKURU ichunguze
KIONGOZI wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi, amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Robanda wilayani Serengeti, Mara baada ya kutilia mashaka thamani ya fedha zilizotumika kugharimia ujenzi huo.

Badala yake, Kiongozi huyo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Serengeti, kuchunguza mwenendo wa ujenzi, usimamizi, matumizi ya fedha na vifaa katika mradi huo, kisha kuwasilisha ripoti kwake kabla Mwenge wa Uhuru haujahitimisha mbio mkoani Mara - Juni 27, mwaka huu.

“Tumekagua jengo la bwalo hili, lakini pia nyaraka kuona kama thamani iliyotumika kujenga inaendana na bwalo lenyewe, usimamiaji na ubora wa jengo lenyewe,” amesema Luteni Josephine mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo Juni 22, 2021.

Amefafanua kuwa katika ukaguzi huo amebaini kuwa Mhandisi hakupima ubora wa vifaa vilivyotumika, kwani vyote havikidhi viwango vya serikali na hadhi ya jengo linalotumiwa na watoto, lakini pia hakuna mihtasari ya vikao vilivyoidhinisha matumizi ya fedha.

“Kingine tulitarajia kukuta mchanganuo wa vifaa vilivyonunuliwa na hakuna uwazi katika hilo, pia hakuna barua za mapokeo ya fedha, ripoti ya ukaguzi wa jengo kutoka kwa mhandisi hakuna. Tuliambiwa tuje kukagua jengo ambalo limekamilika, lakini tumeambia hakuna umeme, vyoo na sehemu za kunawia mikono.

“Basi kutokana na kasoro hizo, Mwenge wa Uhuru umekuwa na mashaka na usimamizi na matumizi ya fedha katika jengo hili, hivyo basi Mwenge wa Uhuru una maagizo yafuatayo:

“Kutafuta na kupata ripoti na majibu yake, ufuatiliaji wa fedha zilizokuwa zikitolewa au kupokelewa kwa namna gani, kuchunguza gharama halisi iliyotumika katika ujenzi huu, Mhandisi atoe maelezo kwanini hakufanya upimaji wa vifaa vilivypotumika kujenga bwalo hili.

“Kufikia jioni [ya Juni 22, 2021] tunaomba kupata muhtasari wa kilichoanza kufanyika katika uchunguzi huu na baadaye uchunguzi utaendelea na ukikamilika ripoti ipelekwe sehemu husina na Mwenge wa Uhuru upewa taarifa kabla ya kuondoka mkoa wa Mara kwenda mkoa mwingine,” ameagiza Luteni Josephine.

Awali, Kiongozi huyo wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021, ameelezwa kuwa hadi sasa ujenzi wa bwalo hilo umegharimu Sh milioni 94.518 zilizotokana na mapato ya ndani ya Serikali ya Kijiji cha Park Nyigoti, na kwamba kazi zilizosalia ni uwekaji wa umeme, ujenzi wa choo na sehemu ya kunawia mikono.

(Imeandikwa na Mara Online News)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages