NEWS

Thursday 8 July 2021

FZS yakutanisha wadau kutafuta suluhisho la migogoro baina ya wanyamapori na binadamu



SHIRIKA la uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) limewakutanisha wadau mbalimbali, katika warsha ya siku mbili ya kutambulisha mradi wa kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu kwenye eneo la Ikona WMA wilayani Serengeti, Mara.

Akifungua warsha hiyo mjini Mugumu leo Julai 8, 2021, Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, ameipongeza FZS - akisema hatua hiyo itasaidia kupata suluhisho la migogoro hiyo katika eneo hilo.
Qamara akifungua warsha hiyo

“Tatizo la migogoro baina ya wanyamapori na binadamu ni kubwa wilayani Serengeti, lazima mikakati na hatua kama hizi za FZS zichukuliwe kukabiliana nalo,” amesema Qamara.

Meneja Mradi wa FZS, Masegeri Rurai ametaja malengo makuu ya warsha hiyo kuwa ni kupeana uelewa wa pamoja na kutambulisha mkakati wa kitaifa kuhusu masuala ya migogoro baina ya wanyamapori na binadamu.


Masegeri Rurai akiwasilisha mada

Rurai ametaja malengo mengine kuwa ni kuonesha juhudi zinazofanywa na FZS katika kupunguza migogoro baina ya wanyamapori na binadamu, na kupata maoni na mapendekezo ya wadau hao juu ya suluhisho la kudumu la migogoro hiyo.

“Lengo la FZS ni kujenga uwezo wa wadau kushiriki kikamilifu katika kusimamia maliasili, uhifadhi na maendeleo endelevu,” amesema Rurai.



Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Antonia Raphael naye amepongeza juhudi zinazofanywa na FZS katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu dhidi ya wananchi.

“Tunafarijika sana kama wizara na serikali kwa hili linalofanyika kuzuia tembo, ni mchango mkubwa sana kwa serikali,” amesema Antonia.

Antonia akiwasilisha mada

Aidha, katika wasilisho lake kuhusu mikakati ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, Antonia ametaja sababu kuu za migongano baina ya wanyamapori na binadamu kuwa ni ongezeko la idadi ya watu sambamba na shughuli zao, kama vile makazi, kilimo na ufugaji.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni kuzibwa kwa shoroba na maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori kutokana na shughuli za kibinadamu na uingizaji mifugo katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori - unaosababisha tembo kutoka hifadhini kwenda kusababisha madhara kwa wananchi na mali zao.



“Maeneo ya shoroba za wanyamapori ni maeneo ya wazi yanayotumiwa na wanyamnapori kupita, au kutoka eneo moja lililohifadhiwa kwenda eneo jingine lililohifadhiwa.

“Shoroba na maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori ni muhimu kwenye mfumo wa ikolojia, kwa ajili ya mahitaji muhimu kama maji, chakula, kuzaliana, makazi na usalama,” amesema Antonia.



Pamoja na mambo mengine, wadau hao wanajadiliana juu ya mikakati ya udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, hasa tembo na simba.

Baadhi ya wadau wanaoshiriki wardha hiyo ni kutoka Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Ikona, TANAPA, TAWA, TAWIRI, WWF na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages