NEWS

Tuesday 19 October 2021

Ruhusa ya buffer zone: Mifugo ya wananchi Tarime Vijijini yakamatwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Waitara azungumza
IKIWA ni siku tatu zimepita, baada ya Serikali kutangaza kuruhusu wakazi wa vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya za Serengeti na Tarime, kutumia eneo kinga (buffer zone) la hifadhi hiyo, ng’ombe 30 na kondoo 10 wa mkazi wa kijiji cha Karakatonga wamekamatwa na wahifadhi.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Vitus Mwera amezungumza na Mara Online News kwa njia ya simu jioni ya leo Oktoba 19, 2021 na kuthibitisha kukamatwa kwa mifugo hiyo.

“Ng’ombe 30 na kondoo 10 waliokamatwa ni mali ya mzee Igayi Mororo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Karakatonga wilayani Tarime,” Mwera amesema.

Inaelezwa mwanakijiji huyo alipoulizwa na wahifadhi sababu ya kuingiza na kuchunga mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, amejitetea kuwa ni baada ya kusikia Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ametangaza kuwa Serikali imewaruhusu kuchunga maeneo waliyokuwa wakizuiwa.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu leo jioni, Waitara amekana kutangazia mwananchi yeyote kutumia buffer zone kabla wataalamu hawajaenda kuonesha mpaka wa hifadhi hiyo, kama ilivyoelekezwa na Serikali.

Katika mazungumzo hayo, Waitara amesema taarifa alizonazo ni kwamba mifugo hiyo imekamatwa ikichunga ndani ya hifadhi.

“Wamenipigia simu asubuhi wakasema hiyo mifugo imekamatwa kwenye eneo la hifadhi… wala hakuna mtu aliyewambia waanze kupeleka ng’ombe kwenye buffer zone,” Waitara ameiambia Mara Online News.

Waitara pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Oktoba 16, 2021, mbunge huyo alihutubia mkutano wa hadhara wa katika maeneo ya vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wilayani Tarime na kuwajuza kuwa Serikali imeruhusu wananchi wa vijiji hivyo kutumia eneo kinga la hifadhi hiyo.
Waitara akihutubia mkutano huo

Taarifa zaidi zilizoifikia Mara Online News hivi punde, zimesema ng'ombe wengine kadhaa wamekamatwa na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika kijiji cha Nyandage ambacho pia kipo jirani na hifadhi hiyo upande wa Tarime.

"Mimi nimekamatiwa ng'ombe watano leo asubuhi wakiwa wanaenda kupata chumvi katika eneo la Gong'ora," Mkazi wa kijiji hicho, Mkami Mogesi amesema.

Wananchi hao wana hofu kuwa huenda mifugo iliyokamatwa ikataifishwa, kwa mujibu wa sheria za uhifadhi.

"Hapa vijijini hali ni tete, watu wamekamatiwa mifugo, tuna hofu inaweza kutaifishwa. Kuna mzee mmoja aliwahi kufariki dunia baada ya ng'ombe wake kukamatwa na kutaifishwa," Mmoja wa viongozi kutoka maeneo hayo amesema.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumtafuta msemaji wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ajili ya kuzungumzia matukio ya kukamatwa kwa mifugo hiyo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages