MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi (pichani juu), ameutangazia umma kwamba kutakuwepo na usalama wa kutosha na upatikanaji wa huduma zote muhimu wakati wote wa ugeni wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, atawasili na kupokewa mkoani Mara Februari 4, mwaka huu, kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala, yatakayofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Karume mjini Musoma siku inayofuata.
Kwa mujibu wa RC Hapi, Februari 6 na 7, mkuu huyo wa nchi atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika Manispaa ya Musoma, Bunda, Musoma Vijijini na Butiama - ambako pia atazuru katika kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Mkoa wetu tumejipanga vizuri, tuwahakikishie Watanzania na wageni wetu wote watakaokuja katika mkoa wetu, tumejipanga vizuri kuhakikisha usalama wa kutosha unakuwepo na tunaweza kuhimili ugeni mkubwa wa watu ambao utafurika katika mji wetu” amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Musoma leo.
RC Hapi ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuanzia kwenye mapokezi ya Rais Samia, sherehe za CCM na maeneo yote ambayo atapita, kuzindua miradi na kuhutubia mikutano ya hadhara mkoani Mara.
Kuhusu upatikanaji wa huduma, amesema watoa huduma zote muhimu, zikiwemo za chakula, usafiri, malazi na burudani wamejipanga kwa ajili ya kuhudumia wateja saa 24. “Hivyo kila mtu atapata huduma wakati wote, hata kama ni usiku wa manane,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha wafanyabiashara mbalimbali kutumia fursa hiyo kutangaza huduma, shughuli na bidhaa zao, lakini pia kukuza uchumi wao katika mazingira ya kuvutia wateja.
“Tuboreshe usafi, huduma nzuri, kauli nzuri na uaminifu kwa wageni ili kuupa sifa mkoa wetu ndani na nje ya Tanzania,” RC Hapi amesisitiza.
Mkuu huyo wa mkoa amehitimisha kwa kuhimiza wananchi kuimalisha amani na utulivu kipindi chote cha ugeni huo wa mkuu wa nchi, ambao ameutaja kuwa ni tukio la kihistoria katika taifa letu.
(Habari na picha zote: Christopher Gamaina - Mara Online News)
No comments:
Post a Comment