RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, ambapo amemteua Dkt Pindi Hazara Chana (pichani juu) kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Kabla ya uteuzi huo, Dkt Pindi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu).
Rais Samia Suluhu Hassan
Hivyo kwa uteuzi huo wa leo, Dkt Pindi amechukua nafasi ya Dkt Damas Daniel Ndumbaro ambaye Rais Samia amemteua kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kwa uteuzi huo wa leo, Dkt Ndumbaro amechukua nafasi ya George Boniface Simbachawene, ambaye ameteuliwa na Rais Samia kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu).
“Mabadiliko haya yanaanza mara moja,” imehitimisha taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus jijini Dodoma, leo jioni.
#MaraOnlineNews-Updates
No comments:
Post a Comment