MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wamekumbushwa wajibu wa kusaidia walimu kuhamasisha wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wawapo shuleni.
Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Dkt Vicent Mashinji (aliyesimama pichani juu) amesisitiza suala hilo katika kikao cha baraza la madiwani hao kilichofanyika mjini Mugumu, juzi.
“Madiwani tumieni ushawishi wa kisiasa kuhamasisha wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi, hasa wa shule za msingi wawapo shuleni,” Dkt Mashinji amesisitiza.
Amesema wanafunzi wanaopata chakula shuleni wanakuwa na nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika masomo na mitihani ya kitaifa, ukilinganisha na wasiopata.
Kwa upande mwingine, DC huyo amewataka madiwani hao kushirikiana na viongozi wa serikali katika mwelekeo wa kuleta maendeleo ya wananchi, badala ya kutoa kauli za kukinzana.
Amekemea viongozi wa kisiasa waliojaribu kudhoofisha shughuli ya upandaji miti katika hifadhi ya bwawa la maji Manchira linalohudumia maelfu ya wakazi wa mji wa Mugumu na vijiji jirani.
“Upandaji miti kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, hivyo viongozi tushirikiane kusimamia utekelezaji wake kikamilifu,” DC Mashinji amesisitiza.
Kwa upande wao, madiwani wa halmashauri hiyo wameitaka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kutofumbia macho watumishi watovu wa nidhamu na wasiowajibika vizuri kwa wananchi.
Pia, wameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuwalipa posho wenyeviti wa vitongoji, mitaa na vijiji, kwani wana majukumu makubwa ya kusimamia ulinzi, usalama na kuhamasisha maendeleo ya wananchi.
Kikao hicho kimeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Samson Wambura ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kisangora.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment