Meneja wa Kampuni ya Northern Highlands Coffee, Rishit Radia (wa tatu kutoka kushoto)
Na Mara Online News
-----------------------------
KAMPUNI ya Northern Highlands Coffee imetangaza mipago ya kusaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa kahawa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mipango hiyo ni pamoja na kuwapa wakulima ruzuku ya mbolea na mafunzo ya kilimo bora cha zao hilo, kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).
Akizungumza na Mara Online News ofisini kwake juzi, Meneja wa Kampuni hiyo, Rishit Radia amesema kwa kuanza watawezesha mafunzo ya kilimo chenye tija kwa wakulima na mbolea ya ruzuku.
“Maandalizi ya kuwapa wakulima mafunzo na ruzuku ya mbolea yanaendelea vizuri,” amesema Radia.
Meneja huyo amesema wakulima 300 wa kahawa wanatarajiwa kunufaika na mpango huo kupitia AMCOS za Sirari, Kangariani na Nyantira.
Mpango huo unakuja wakati wakulima wa kahawa wilayani Tarime wakitaja kupanda maradufu kwa bei ya mbolea kama changamoto kubwa inayowalazimu kutumia mbolea za kienyeji.
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka (katikati) na viongozi wengine wakionesha kahaw inayotengenezwa na kampuni hiyo.
Radia amesema Northern Highlands Coffee kwa sasa inaongoza kwa kutoa bei ya juu kwa wakulima, kuliko wanunuzi wengine wa kahawa wilayani Tarime.
“Mbali na mpango huo wa mafunzo na ruzuku ya mbolea, tunatoa bei nzuri kwa wakulima kuliko wanunuzi wengine,” amesema.
Taarifa zilizopo zinaonesha kampuni hiyo inaongoza kwa kutoa bei nzuri kwa wakulima hivi sasa.
Kampuni ya Northern Highlands Coffee inanunua na kuchakata kahawa ambayo soko lake linakuwa kwa kasi ndani na nje ya nchi.
Mfano Meneja Radia amesema soko la kahawa inayochomwa (roasted) linakuwa kwa kasi ndani na nje nchi.
Kampuni hiyo inaahidi kuendelea kuongeza thamani ya zao hilo la biashara ambalo ni tegemeo la mamia ya wakulima wilaya Tarime na maeneo mengine ya Kanda ya Ziwa.
Kahawa aina ya Arabica inayozalishwa Tarime inaelezwa kutamba katika soko la dunia kutokana na kuwa na muonjo bora na wenye radha halisi (natural taste), kwa mujibu wa watalaamu wa kahawa Tanzania.
No comments:
Post a Comment