NEWS

Sunday 5 June 2022

Tegesha mgodi wa North Mara kutolipwa bilioni 20/-, wadai halali waanza kucheka, kulipwa Sh bilioni 26



WATU zaidi ya 5,000 hawatalipwa fidia ya shilingi bilioni 20 baada ya kubainika walitegesha nyumba na mazao ikiwemo miti kwenye eneo lililozuiwa kisheria kuendelezwa, ili kupisha shughuli za Mgodi wa Dhababu wa North Mara.

Kwa mujibu wa Mthamini wa Serikali, Rashid Magetta, watu hao walitegesha vitu hivyo katika kijiji cha Komarera wilayani Tarime, baada ya tangazo la Serikali la zuio la kuendeleza eneo hilo kutolewa kwa mujibu wa sheria.

“Uthamini uliofanyika ni wa shilingi bilioni 46, lakini imebainika kuwa kati ya hizo, shilingi bilioni 20 ni tegesha na hawatalipwa,” Magetta ameiambia Mara Online kijijini Komarera, juzi.

Amesema watu 6,847 ambao madai yao ni halali kutokana uthamini huo watalipwa shilingi bilioni 26 na kwamba tayari ulipaji umeshaanza.

“Hadi sasa watu 2,058 wamelipwa shilingi bilioni 8.9 na ulipaji unaendelea,” amesema Magetta.

Mara Online News imeshuhudia baadhi ya nyumba zilizobainika kutegeshwa - yakiwemo majengo yaliyodaiwa kuwa ni ya madhehebu ya dini.

Mojawapo ya majengo yaliyobainika kutegeshwa kijijini Komarera ni pamoja na hili lililodaiwa kuwa ni la dhehebu la dini.

Kulingana na Mthamini huyo wa Serikali, majengo hayo yalijengwa baada ya tangazo la katazo la kuendeleza eneo hilo kutolewa Mei 28, 2020.

Amefafanua kuwa hata nyumba za wenyeji ambazo ziliongezwa baada ya tangazo la katazo hilo lililotolewa kwenye mkutano wa hadhara wa kijiji na kubandikwa kwenye ubao wa matangazo wa ofisi ya Serikali ya Kijiji hazitalipwa.

“Nyumba halali zitalipwa lakini zilizoongezwa hazitalipwa. Picha za setilaiti zinaonesha kila kitu kilichokuwepo wakati tangazo la katazo la kuendeleza eneo la mradi linatolewa,” amesisitza Magetta.

Alipoulizwa hatima ya majengo yaliyobainika kutegeshwa mara baada ya ulipaji wa fidia kukamilika, Mthamini huyo wa Serikali amesema zitabomolewa kwa kuwa ujenzi wake ulikiuka sheria.

“Picha za setilaiti zinaonesha hizi nyumba hazikuwepo wakati wa katazo. Lakini ukiwahi ukajenga nyumba au kuendeleza eneo kabla ya tangazo la katazo huwa hatuna ujanja lazima walipwe,” amesema Magetta.
Mthamini Magetta akionesha baadhi ya nyumba zilizotegeshwa kijijini Komarera.

Kwa upande mwingine, majaribio ya kutegesha mashamba ya miti yameonekana katika eneo jingine lenye ukubwa wa ekari 262 kijijini Komarera, ambalo pia mgodi wa North Mara unalihitaji kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.

Zuio la kuendeleza eneo hilo lilitangazwa na Serikali kwa wakazi wa kijiji hicho Juni 1, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Komarera, Nyamaganya Marwa amekiri kuwa baadhi ya watu wamebainika kuanza kujihusisha na vitendo vya kupanda miti katika eneo hilo.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amekemea vitendo hivyo akisema havikubaliki kwani vinakiuka zuio la Serikali lililotangazwa kwa mujibu wa kisheria.

“Hao wanaofanya vitendo hivyo kwa sasa wanakosea, tumeshawazuia kwamba kufanya hivyo ni nje ya utaratibu,” amesema Marwa katika mazungumzo na Mara Online News, juzi.

Shehena ya miche yanaswa
Baada ya kutolewa kwa tangazo la kuzuia kuendeleza eneo jingine kijijini Komarera mapema mwezi huu, harakati za kutegesha zimeripotiwa kuanza, huku miche mingi ikisombwa kwenda kupandwa eneo hilo.

Mwenyekiti Marwa amesema idadi kubwa ya miche imekamatwa ikipelekwa kupandwa kwenye eneo hilo kinyume na utaratibu.

“Kinachoendelea kwenye eneo ambalo limezuiwa kuendelezwa kwa sasa ni dhambi na pengine hiyo sasa ndiyo inaweza kuitwa ni tegesha,” amesema Marwa.

Mwenyekiti huyo amesema nguvu kubwa inatumika kuzuia upandaji miti katika eneo hilo ambalo limetangazwa kuwa kwenye mradi.

“Tunatumia nguvu nyingi na tunakamata miche ya miti,” amesema Marwa - akitolea mfano lori lililokamatwa kijijini hapo hivi karibuni likiwa limepakia miche ya miti ikipelekwa kupandwa katika eneo jipya linalohitajiwa kwa shughuli za mgodi.

Ameongeza “Tunakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivi ili wasiharibie wengine wenye mashamba halali wakati wa uthamini kwenye eneo hilo.”

Aina za miti inayotajwa tumika kama ‘dili’ kutegesha ni pamoja na miembe, mikorosho na seregina.

Uchunguzi uliofanywa na chombo hiki umebaini kuwa mazao mengi ikiwemo miti hiyo yanapandwa bila kuzingatia kanuni za kilimo bora, kwa lengo la kuwezesha wanaotegesha kuvuna mamilioni ya fedha kutoka mgodi wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.


Inaelezwa kuwa baadhi ya watu wanaotegesha wanakaribishwa na wanavijiji wenyeji na wamepewa jina la chomoa.

“Chomoa ni wale ambao wanaingia makubaliano na wenye ardhi kupanda mazao au miti, hivyo wakati wa kulipwa wenye ardhi wanalipwa kutokana na ukubwa wa ardhi yao na wenye mazao au miti hulipwa fidia ya miti au mazao,” kimesema chanzo chetu cha habari kutoka eneo hilo.

Mthamini Magetta amesema miongoni mwa mambo yanayozingatiwa wakati mgodi unahitaji eneo jipya kuwa ni uhamasishaji ambao pia humhusisha Mkuu wa Wilaya.

“Baada ya uhamasishaji sasa tunaingia field ndio tunakutana na changamoto nyingi, yaani nyumba zinanyanyuliwa usiku na mchana,” amesema.

Biashara hiyo ya tegesha inachangamka mara tu baada ya taarifa za eneo linalohitajika kwa ajili ya shughuli za mgodi kuvuja au kutangazwa rasmi.

“Hili suala huwa ni ngumu. Kwanza wakati mwingine taarifa zinavuja na kufanya watu kuanza kuendeleza maeneo yanayohitajika na wengine wanajenga majengo, au kupanda mazao au miti na kupata hasara baada ya kujikuta kuwa wapo nje ya eneo la mradi,” kimedokeza chanzo chetu kingine.

Hadi sasa mgodi huo umeshatumia mabilioni ya fedha kulipa fidia kwa maelfu ya wananchi wanaohamishwa kupisha shughuli za mgodi, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikiripotiwa kuingia mifukoni mwa watu ambao sio wazaliwa wa vijiji vinavyouzunguka.

“Lengo la tathmini na kulipa fidia huwa ni kuwahamisha wazawa lakini sasa fedha nyingi inalipwa kwa tegesha ambao hulipwa na kukimbia,” amesema Magetta.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara haufurahishwi na hali hiyo ya watu ambao sio wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo kuendelea kulipwa mabilioni ya fidia kutokana na vitendo vya kutegesha.

“Tunaotaka kuwalipa ni wananchi wazawa, kwanini watu wengine ambao ni wakazi wa mikoa mingine nje ya Mara, mfano Dar es Salaam, Mwanza na maeneo mengine wanahujumu uchumi wa wananchi wazawa?” amehoji Afisa Mwandamizi wa mgodi huo katika idara ya uhusiano.

Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Komarera, Mussa Raphael, kijiji hicho kina wakazi 10,938 (wanawake 5,835 na wanaume 5,103).

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Marwa amebainisha kuwa wananchi waliofanyiwa tathmini ya ardhi, nyumba na mashamba yao kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 652 kijijini hapo ni zaidi ya 6,800.

Kwa takwimu hizo, Mwenyekiti Marwa ametofautiana na Mthamini wa Serikali, Magetta ambaye amesema watu waliofanyiwa tathmini hiyo kijijini hapo ni zaidi ya 11,000 wakiwemo 5,000 waliobainika kutegesha nyumba na mazao mbalimbali.

Hata hivyo kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo hakubaliani na kitendo cha kuwaondoa watu 5,000 kwenye suala la kulipwa fidia, akisema uthamini ulicheleweshwa, hivyo kusababisha baadhi ya wanakijiji kuendeleza maeneo yao.

“Mthamini wa kwanza alisitisha uthamini na kuondoka bila kutoa taarifa, hivyo baada ya kuona umepita muda mrefu bila taarifa yoyote tukajua ule mpango umekufa, watu wakaanza kuendeleza maeneo yao, maisha yakaendelea,” amesema Marwa.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages