NEWS

Sunday 31 July 2022

Kwanini Adam Malima anafaa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza



Adam Kighoma Malima

Na Sauti ya Mara Digital
------------------------------

WIKI iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alimhamisha Adam Kighoma Malima kutoka Mkoa wa Tanga kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Mwanza ni jiji lenye mambo mengi ya kihistoria yanayoweza kutumika katika kuimarisha uchumi, utalii wa ndani na wa kigeni, miongoni mwa sekta nyingine.

Mkoa wa Mwanza umebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii kama vile Ziwa Victoria, Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane, Makumbusho ya Wasukuma ya Bujora, jiwe lilalocheza Ukerewe, visiwa vya aina yake na makazi ya watu milimani.

Malima amepelekwa kuongoza mkoa wa Mwanza akiwa tayari ameshatangazwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Balozi wa Heshima wa Utalii nchini.

Wizara ilimtunuku Malima ubalozi huo baada ya kuonekana ni mmoja kati ya wakuu wa mikoa wanaofanya vizuri katika sekta ya utalii nchini.

Hakika mkoa wa Mwanza sasa umepata Mkuu wa Mkoa anayeufaa, pengine kuliko wengine wote waliokwisha kuuongoza.

Malima anaamini kuwa ili kupata mafanikio mazuri katika utalii, lazima kufanya maamuzi magumu na kutoingiza siasa kwenye masuala ya uhifadhi.

Inawezekana dhana hiyo ambayo Malima ameijenga ndiyo imemshawishi Rais Samia kumhamishia mkoani Mwanza kwa matarajio ya kuleta mabadiliko chanya na yenye tija katika sekta ya utalii na nyingine kama vile biashara, uvuvi na viwanda.

Viongozi wa ngazi ya juu na hata wananchi wa kawaida wanatambua uwezo, ujasiri na umahiri wa Malima katika utendaji kazi, ikiwemo ya kuhamasisha utalii, uhifadhi na hata kilimo cha mazao ya kimkakati.

Miongoni mwa mifano hai ya umahiri wa Malima katika utendaji kazi, ni ule wa kuwa mstari wa mbele kutangaza utalii wa ndani na uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti hadi ikifanikiwa kushinda Tuzo ya Hifadhi Bora barani Afrika kwa miaka mitatu mfululizo (2019, 2020 na 2021).

Hivyo matarajio ya wadau wengi ni kwamba sasa mkoa wa Mwanza unakwenda kuchanua zaidi, hasa katika sekta za utalii, uhifadhi na biashara.

Kwamba changamoto zinazokabili sekta za utalii, uhifadhi, uvuvi, biashara na kilimo cha mazao kama vile pamba na mpunga mkoani Mwanza, sasa zitapata ufumbuzi thabiti chini ya uongozi wa Malima.

Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane na hoteli za kifahari ni miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyopo Mwanza vinavyohitaji nguvu ya ziada kuvitangaza ili kushawishi wageni wengi kuvitembelea na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi mkoani humo.

Hakuna shaka kwamba Malima atatumia vipaji vyake vya ubunifu na diplomasia kuhamasisha ufanisi katika sekta hizo kwa manufaa ya wana-Mwanza na taifa kwa ujumla.

Lakini pia, Malima hataiweka kando sekta ya michezo kwani ni mdau na mpenzi mkubwa wa sekta hiyo, hususan mpira wa miguu (soka).

Mapenzi ya Malima kwenye soka yamekuwa yakidhihirika wazi na hata alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara miaka kadhaa iliyopita, alishiriki kwa hali na mali hadi kuwezesha Timu ya Soka ya Biashara United “Wanajeshi wa Mpakani” kupanda Ligi Kuu.

Mbali na sekta za utalii, uhifadhi, biashara, viwanda, uvuvi, kilimo na michezo, Malima kama Mkuu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, atarajiwe pia kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha usalama wa raia na mali zao mkoani Mwanza, ili kuwezesha wananchi kuishi na kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu.

Hata manung’uniko yaliyopo miongoni mwa wananchi kwamba baadhi ya askari polisi waonea na kubambika raia kesi ‘nzito’, inatarajiwa yatapungua kama si kumalizika mkoani Mwanza chini ya uongozi wa Malima.

Jambo hilo ni muhimu kushughulikiwa kwani kumekuwepo na malalamiko kuwa baadhi ya watuhumiwa wa uhalifu wamekuwa wakiteswa kwa kupigwa na askari polisi, kudhihakiwa, kuombwa rushwa, kunyang’anywa baadhi ya mali zao, kunyimwa haki za kudhaminiwa na kuwasiliana na ndugu zao katika vituo vya polisi mkoani Mwanza.

Watu wengi tuna imani kubwa kwamba Malima ana uwezo na mbinu za kukomesha vitendo vya uonevu na unyanyasaji dhidi ya raia wasio na hatia ambavyo vimekuwa vikiendekezwa na askari polisi wachache mkoani Mwanza.

Itoshe tu kuamini kwamba Mkuu wa Mkoa, Adam Kighoma Malima ni jembe thabiti na atakuwa chachu ya maendeleo ya kisekta mkoani Mwanza, huku utalii ukipewa kipaumbele ili kukidhi matarajio ya Rais Samia ambaye kwa makusudi makubwa, ameweza kuandaa na kuzindua Filamu ya The Royal Tour kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages