NEWS

Saturday 6 August 2022

Shirika la VSO lawezesha vijana, wanawake na wenye ulemavu kutambua haki zao, fursa za kiuchumiNa Mara Online News
----------------------------

SHIRIKA la VSO limewapatia viongozi wa vikundi maalumu mafunzo ya kuwezesha makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutambua mifumbo ya kutetea haki na fursa za kiuchumi.

Mafunzo hayo yamefanyika katika kijiji cha Mjini Kati kilichopo kata ya Matongo wilayani Tarime, juzi.

Yameendeshwa na Mshauri wa stadi za maisha na mafunzo ya wanawake na watu wenye ulemavu kutoka Shirika la VSO, Photunatus Nyundo.

“Tunajengea uwezo makundi haya ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu waweze kutambua mifumo mbalimbali ya kutetea haki, fursa za uchumi zilizopo, hususan usalama na ulinzi wa chakula, ulinzi wa ajira na kipato,” amesema Nyundo.

Amesema viongozi waliopata mafunzo hayo watayaeneza na kufanya uchehemuzi ili kusaidia jamii iweze kujua haki zao kutokana na miongozo na sera mbalimbali za serikali.

VSO ni Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitolea, ambapo kidunia makao makuu yapo nchini Uingereza na hapa Tanzania makao makuu yake yapo jijini Dar es Salaam.

Kwa sasa shirika hilo linatekeleza mradi wa miaka mitatu wa CLARITY kwa kusaidiana na taasisi rafiki ambazo ni TWCC na LEAT katika mikoa ya Geita na Mara.

“Katika mkoa wa Mara tunatekeleza programu ya kuhamasisha uwajibikaji, uwazi na kujitolea kwa jamii,” amesema Nyundo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages