Waziri Dorothy Gwajima
Na Mara Online News
---------------------------
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt Dorothy Gwajima (pichani juu) amezungumzia tukio la Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Mara, Dkt Juma Mfanga kumshambulia mtumishi wa kike usiku katika Hospitali ya Serikali Nyamwaga wilayani Tarime na kutaka taratibu za kisheria kufuatwa.
“Hatua ya kwanza tukio liripotiwe kwenye vyombo vya sheria, kisha vyombo vitasema class, yaani aina ya tukio hilo kama ni ukatili wa kijinsia au aina gani,” Waziri Gwajima ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo mchana.
Waziri Gwajima alikuwa akijibu swali aliloulizwa na Mara Online News la kutaka kujua kauli yake juu ya tukio hilo - kama Waziri mwenye dhamana ya kutetea usawa na kupinga ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kuwa baada ya tukio hilo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mawaziri wa kisetka, yaani wa TAMISEMI, Utumishi, Afya na Maenedeleo ya Jamii wanaweza kutoa tamko.
Hata hivyo, Waziri huyo amesisitiza kuwa ukatili hautakiwi kwenye jamii mahali popote pale.
Mara Online News imeendelea kuandika habari za tukio hilo zinazoeleza kuwa siku chache zilizopita, Dkt Mfanga alifika katika Hospitali ya Nyamwaga usiku na kuzusha mvutano mkubwa wa mazungumzo na mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo.
Inaelezwa kuwa wakati wa mvutano huo, RMO huyo alimshambulia kwa kumsukuma mtumishi huyo (jina lipo) hadi akaanguka na kuumia sehemu ya kichwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya shambulio hilo mtumishi huyo alisindikizwa na wenzake kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Nyamwaga ili kupata PF3 kwa ajili ya matibabu.
Taarifa zinasema Dkt Mfanga alimuomba msamaha mtumishi huyo akakubali kumsamehe na hivyo suala hilo likaishia hapo kabla ya kuingizwa kwenye kitabu cha malalamiko.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa baada ya maafikiano hayo, RMO huyo baadaye aliwafuata baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo na kutoa vitisho, vikiwemo vya kusudio la kuwahamishia nje ya mkoa wa Mara.
Taarifa zaidi kutoka Hospitali ya Nyamwaga zinasema baada ya tukio la kushambuliwa, mtumishi huyo (jina lipo) aliripoti katika kituo cha polisi Nyamwaga kutoa taarifa, lakini juhudi zilifanyika kumnusuru RMO huyo dhidi ya kashfa hiyo.
“Tukio lilitokea usiku, akaenda akaripoti polisi, RMO akapigiwa simu lakini hakufika, akaahidi kuwa atakwenda asubuhi. Kesho yake asubuhi alikwenda wakakaa kikao kumuomba asiendelee na kesi mbele ya mabosi wake ambao ni RMO mwenyewe, Kaimu Mganga Mkuu na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyamwaga.
“Unategemea angekataa ili kuendelea na kesi mbele ya mabosi wake,” amedokeza mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo ambaye ameeleza kuchukizwa na tukio hilo.
Mmoja wa madaktari wa Serikali amesema “Ilitakiwa RMO awekwe lock up (rumande) na kuchukuliwa hatua za kisheria. Huu ni ukatili wa kijinisia wa kumshambulia mtumishi tena wa kike akiwa kazini usiku.”
Mbali na kuishia juu kwa juu katika Kituo cha Polisi Nyamwaga, taarifa za tukio hilo ziliripotiwa pia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka serikalini.
Inadaiwa kuwa Dkt Mfanga amekuwa akilindwa na mmoja vigogo wizarani na kwa muda mrefu sasa, amekuwa akinyanyasa watumishi wa afya katika halmashauri za mkoa wa Mara na kuwavunja moyo wa kuhudumia wagonjwa.
“Kwa mfano kuna mtumishi wa kituo cha afya Magoma wilayani Tarime ambaye amelazimika kuacha kazi kutokana na maneno ya kuudhi yakiwemo matusi ya nguoni na vitisho kutoka RMO huyo.
“Sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kuhusu namna ya kumwajibisha mtumishi anapoonekana kufanya kosa, lakini huyo RMO amekuwa akienda kinyume na miongozo hiyo ya Serikali,” kimedokeza chanzo chetu cha habari.
Baada ya taarifa za tukio hilo kuripotiwa na Mara Online News tangu juzi, watumishi wa afya kutoka hospitali mbalimbali za mkoani Mara wamepiga simu kwenye chumba cha habari na kufunguka jinsi wanavyonyanyaswa na Dkt Mfanga.
Wataalamu wa afya wa Serikali wanasema vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya matusi vinavyofanywa na RMO huyo ni hatari kwa utoaji wa huduma bora za matibu katika mkoa wa Mara.
“Ameumiza watu wengi kimwili na kisaikolojia, siyo Tarime tu, hata Musoma Vijijini mpaka ofisini kwake kuna watumishi wanalalamika kunyanyaswana na RMO huyo.
“Mtumishi wa afya akishakuwa disturbed anakosa molari ya kuhudumia wagonjwa. Hii ni hatari sana, mamlaka za uteuzi zitazame upya vigezo vya kuwapa watu madaraka ya RMO.
“Kosa la kufanya shambulio la mwili kwa mtumishi mwenzake ni kati ya makosa makubwa yanayoweza kumfukuzisha kazi.
“Hakuna mahali RMO anaruhusiwa kufanya kazi usiku bila kumtaarifu Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Wilaya husika, shambulio alilofanya ni kosa la jinai,” amesema mmoja wa maktari wandamizi mkoani Mara.
Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu juzi saa tano asubuhi, Dkt Mfanga alidai kuwa alikuwa kikaoni na kuahidi kupiga simu baada ya kikao.
Hata hivyo, baada ya Mara Online News kusubiri hadi saa 10 jioni iliamua kumpigia Dkt Mfanga simu tena ambapo iliita bila kupokewa.
Hivyo, Mara Online News iliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms), ndipo baadaye akajibu kwa kifupi “Fika ofisini… huyo aliyekutuma mwambie akuwezeshe na nauli”.
Alipotafutwa na Mara Online News kwa njia ya simu ili kuzungumzia suala hilo leo asubuhi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Benjamin Oganga amesema amepata taarifa za tukio hilo kupitia kwenye chombo cha habari na kuahidi kilitolea ufafanuzi leo mchana.
Hata hivyo, Kaimu RAS huyo ambaye leo pamoja na mambo mengine alikuwa kwenye mapokezi ya Katibu Tawala mpya wa Mkoa wa Mara, Msalika Robert Makungu, hadi habari hizi zinakwenda mitamboni jioni ya leo hakuweza kutimiza ahadi hiyo ya kutoa ufafanuzi wa tukio hilo.
Katika hotuba yake kwenye hafla ya mapokezi yake leo, RAS Makungu amewataka wafanyakazi mkoani Mara kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Bado Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata Mawaziri wenye dhamana, akiwemo Ummy Mwalimu wa Afya na Innocent Bashungwa wa TAMISEMI, kwa ajili ya kuzungumzia suala la tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa RMO Mkoa wa Mara, Dkt Mfanga.
Jumatatu iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya kuapisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wapya, aliwasisitiza viongozi wote wa umma kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment