Na Mwandishi Wetu, Mwanza
----------------------------------------
MKURUGENZI wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (pichani), amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.
“Hii inaonesha imani kubwa waliyonayo wakuu wa vyuo vya ufundi katika mikoa yetu ya Kanda ya Ziwa,” Hezbon alisema muda mfupi baada ya uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa VETA Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, Ijumaa iliyopita.
Hii ni mara ya pili kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kumchagua Hezbon kushika wadhifa huo, baada ya kuonekana kufanya vizuri katika awamu ya kwanza.
Hezbon anaongoza Taasisi ya PMF inayoendesha programu ya mafunzo ya ufundi na taaluma mbalimbali kwa mamia ya vijana kutoka mikoa tofauti nchini, kupitia Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime.
“Vijana waliopata daraja la nne na alama sifuri wana fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili wasijione wametengwa… kupitia vyuo vya ufundi wanaweza kupanda hadi chuo kikuu na hatimaye kuajiriwa, au kujiajiri kutokana na fani walizosoma.
“Tunahamasisha vijana baada ya kumaliza kidato cha nne, wakati wanasubiri matokeo ni vizuri wakajiunga na vyuo vya ufundi wakapata zile fani, matokeo yakitoka yakiwa mazuri, kijana akienda advance (kidato cha tano) akiwa na fani yake kuna sehemu itamsaidia.
“Lakini matokeo yasipokuwa mazuri, ile fani pia anaweza akajiendeleza nayo na baadaye ikamsaidia kujiajiri au kuajiriwa. Kwa hiyo tuhamasishe vijana kuona umuhimu wa kujiunga na hivi vyuo vya ufundi ambavyo kwa sasa vimeunganishwa na NACTE ili kuviboresha kitaaluma,” anasema Hezbon.
Anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuiletea nchi maendeleo ya kisekta, ikiwemo kutoa fursa kwa watoto wa kike kuendelea na masomo baada ya kuwa wamekatishwa kwa kupata ujauzito na kujifungua.
Anasema Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime ni moja ya vyuo vikubwa Kanda ya Ziwa, na tayari kimeanzisha mpango wa kusaidia vijana kusoma bure na kwamba hadi sasa kimeshasaidia vijana zaidi ya 3,000.
“Ninamshukuru na kumpongeza Mama [Rais Samia] kwa kufungua mipaka na kuleta fursa nyingi kwa Tanzania, lakini pia kwa maono makubwa ya kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Tunaona juhudi zake katika shule - ametoa fedha za kujenza madarasa ili kuongeza fursa kwa watoto wengi kupata elimu,” anasema Hezbon.
Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya PMF anaongeza kuwa Rais Samia pia anastahili pongezi kwa kuonesha dhamira ya kuanzisha vyuo vya ufundi kila wilaya nchini.
Chanzo: Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment