NEWS

Saturday 29 October 2022

Umoja wa Madhehebu wafikisha elimu ya tahadhari ya ebola kwa viongozi wa dini TarimeNa Mara Online News, Tarime
------------------------------------------

VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini wilayani Tarime, wamejengewa uwezo wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola, katika semina ya siku moja iliyoendeshwa na Umoja wa Madhehebu ya Dini Tanzania (TIP) kwa kushirikiana na Serikali.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo iliyofanyika mjini Tarime jana Oktoba 28, 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa TIP, Asina Shenduli alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kuhamasisha wananchi kuchukua thadhari ya ugonjwa huo ulioripotiwa kulipuka nchini Uganda.

Shenduli alisema pamoja na kwamba ugonjwa wa ebola haupo Tanzania, TIP imeona ina jukumu la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha hauingii nchini.

“TIP tumekuwa na utamaduni wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mambo mbalimbali nchini, tumesaidi kuhamasisha wananchi kupata chanjo ya UVIKO-19 na sasa tunaisaidia kuhakikisha ugonjwa wa ebola hauingii nchini,” alisema.

Asina Shenduli

Mada ya Shenduli ilijikita zaidi katika kuelimisha viongozi hao wa dini kinachosababisha ugonjwa wa ebola, dalili zake ni nini na namna ya kuchukua tahadhari na kujikinga nao.

Shenduli alitumia nafasi hiyo pia kulishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) kutoa ufadhili wa kuendesha semina hiyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Chipole Mpelembe alisema Serikali imeona umuhimu wa kuunganisha nguvu na viongozi wa dini kupitia semina hiyo ili nao waweze kufikisha elimu hiyo kwa waomini wao na jamii kwa ujumla.

Chipole Mpelembe

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Josephine Ninga alisema wamejipanga kukabiliana na ebola ikitokea imeingia wilayani hapa.

“Sisi kama ofisi ya Mganga Mkuu tumejipanga na tumeshaandaa kambi maalum kama ikitokea tumetapa mhisiwa, na tuna timu ya wataalamu waliopata mafunzo na wako tayari kufanya kazi hiyo,” alisema Ninga.

Josephine Ninga

Viongozi wa dini walioshiriki semina hiyo waliipongeza TIP na Serikali kuchukua tahadhari ya ebola mapema ili kulinda usalama wa afya za wananchi wake.

“Elimu ni muhimu katika kupambana na jambo lolote, Serikali yetu inapenda wananchi wake waishi kwa amani na afya njema, kwa sababu bila kuwa na afya huwezi kufanya jambo lolote, nchi yoyote lazima iwe na watu wenye afya ya kuweza kufanya maendeleo ya kitaifa,” Katibu wa Msikiti wa Buhemba, Abdallah Abdul Msabakwa alisema.

Picha zote na Mara Online News

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages