NEWS

Monday 5 December 2022

Mbunge Waitara awasihi wananchi kuacha kupeleka mifugo kuchunga ndani ya Hifadhi ya SerengetiNa Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (pichani katikati), amewasihi wananchi wa jimbo hilo, hususan wakazi wa vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kuacha kupeleka ng’ombe na mifugo mingine kuchunga ndani ya hifadhi hiyo.

Waitara alitoa wito huo Alhamisi iliyopita kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Masanga, kilomita chache kutoka hifadhi hiyo ambayo imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka minne mfululizo, yaani 2019, 2020, 2021 na 2022.

Mbunge huyo aliwakumbusha wanavijiji kuwa sheria inazuia mifugo kuingia ndani ya hifadhi, ndio maana ng’ombe wanapokamatwa hifadhini mmiliki husika hutozwa faini ya shilingi laki moja kwa kila mmoja, au mifugo yake kutaifishwa na Serikali.

“Mimi sitaki watu wangu wafilisike, ukitaka kumsaidia mtu mwambie ukweli,” Waitara alisisitaza na kuwataka wananchi hao kupuuza maneno ya aliowaita wanasiasa wahuni, ambao hawawambii ukweli kuwa kuchunga mifugo ndani ya hifadhi ni kuvunja sheria.

Aliweka wazi kuwa kuanzia sasa hatahusika kusaidia ufuatiliaji wa mifugo itakayokamatwa ikichunga ndani ya hifadhi hiyo, huku akiwatupia lawama wananchi ambao wamekuwa wakikaidi katazo la kutopeleka ng’ombe hifadhini.

“Kuanzia leo mkichunga kwenye hifadhi, mimi sitaonekana, haitatokea. Haiwezekani kila siku ni kesi. Mimi habari ya kesi sitafanya, mimi nitatetea wanaoonewa. Hifadhi, watu na mifugo yao vyote ni muhimu,” alisisitiza kiongozi huyo wa wananchi.

Alisema hakuna mbunge mwenye nia njema anayeweza kusimama na kuwaelekeza wananchi kuchunga mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa kama Serengeti, akisema wanaoweza kufanya uchochezi huo ni matapeli wa kisiasa.

“Inabidi tuishi kwa akili sana, mkidanganywa mtakuwa maskini. Mimi siwezi kuwadanganya kwamba mwende kuchunga hifadhini. Faini ya kila ng’ombe ni shilingi laki moja, au faini na pamoja mwenye mifugo kufungwa na mifugo yake kutaifishwa,” Waitara aliwambia wananchi hao.

Kuhusu mpaka kati ya wanavijiji hao na Hifadhi ya Serengeti, Mbunge Waitara alisema suala hilo ameshalifikisha kwa viongozi wa juu serikalini na litapatiwa ufumbuzi.

“Hili suala lipo serikalini, tusubiri tutapitia mpaka vizuri, sheria itekelezwe na majadiliano yawepo. Nimepeleka maombi yangu ili tupate namna ya kuishi salama na hifadhi iendelee kuwepo.

“Kwa hiyo ndugu zangu nataka niwashauri vizuri kwamba jambo hili ni la kisheria, nimeshapeleka hoja serikalini. Nimeomba mawaziri waje hapa wafanye mkutano na wananchi tupate ufumbuzi. Hivyo msivamie hifadhi, huo ndio msimamo wangu,” alisisitiza Mbunge Waitara.

Walipoulizwa na mbunge wao huyo kama wamemuelewa na kukubali maelekezo yake ya kuwataka kuacha kupeleka mifungo kuchunga ndani ya hifadhi hiyo, wananchi waliohudhuria mkutano huo walikubali kwa pamoja.

Akihutubia mkutano mwingine wa hadhara kijijini Itiryo siku moja baadaye, Mbunge huyo wa Tarime Vijijini aliwataka wanavijiji kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia za mifugo.

“Watu wameambiwa hii ni sehemu ya kupitisha mifugo, lakini wengine wamekwenda wamepanda katani na wengine wamejenga makazi hapo hapo,” Waitara alisema kwa mshangao na kuongeza:

“Lazima tuambizane maneno magumu, ukivunja sheria, sheria ichukue mkondo wake.”

Inaelezwa kuwa wanavijiji wamekuwa wakiingiza mifugo hifadhini na hivyo kusababisha migogoro kati yao na wahifadhi. Aidha, mifugo imekuwa ikikamatwa, kutozwa faini na kutaifishwa, na hivyo kuongeza umaskini kwa wananchi hao.

Baadhi ya vijiji vya wilayani Tarime vilivyopo jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni Masanga, Kegonga, Nyandage, Karakatonga, Kenyamsabi na Gibaso.

Chenzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages