NEWS

Wednesday 1 March 2023

Kamati ya Siasa CCM yakagua miradi Tarime Vijijini, yatoa siku 3 uezekaji kituo cha afya Bumera ukamilishwe


Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho akitoa maelekezo kwenye mradi wa kituo cha afya Bumera.

Na Mara Online News
-----------------------------------

KAMATI ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime, leo Machi 1, 2023 imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya hiyo (Vijijini).

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, imetoa muda wa siku tatu kwa wasimamizi na mafundi husika kukamilisha uezekaji wa jengo la upasuaji, mama na mtoto katika kituo kipya cha afya kinachojengwa katika kata ya Bumera.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati amesema tayari shilingi milioni 500 zimeshatolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Mara Online News imeshuhudia majengo ya OPD na maabara yakiwa katika hatua za mwisho wa ujenzi.

Muonekano wa mbele wa jengo la OPD kituo cha afya Bumera

Hata hivyo Mkurugenzi Shati amesema hatua mbalimabli zimeanza kuchukuliwa kuhakikisha mradi huo unakamilika kama ilivyopangwa, ikiwemo kumweka pembeni mtumishi anayehusishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyobaini dosari kadhaa.

Kwa upande mwingine, wajumbe wa kamati hiyo wameridhishwa na ujenzi wa chumba cha darasa uliotengewa shilingi milioni 20 za mapato ya ndani, ambao umekamilika na chenji ya shilingi laki tatu kubaki.

Ukaguzi wa miradi ukiendelea

“Kamati ya Siasa tumekagua hili jengo tumeridhika na kazi nzuri iliyofanyika,” Ngicho amesema baada ya kukagua darasa hilo ambalo tayari limeanza kutumiwa na wanafunzi katika Shule ya Msingi Kiterere.

Aidha wajumbe wa kamati hiyo ambao pia wamefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, wamekagua mradi wa maji wa Nyabirongo unaotekelezwa na Bodi ya Maji ya Ziwa Victoria katika kijiji Nyabirongo.

Wajumbe wa kamati wa siasa CCM Tarime wakipata maelezo ya mradi maji Nyabirongo

Ujenzi wa mradi huo ambao umefikia hatua za mwisho kukamilika, utatoa huduma kwa takriban wananchi 3,000 na shule za umma kijijini hapo.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imetembelea Shule ya Msingi ya Mgwera iliyopo kijiji cha Nyabirongo na kuagiza matatizo ya sakafu katika moja ya madarasa na upungufu wa madawati shuleni hapo yatatuliwe haraka.

Kamati hiyo ya siasa itaendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo kesho, huku Mwenyekiti Ngicho akisisitiza kuwa miradi yote ya kimkakati inayogharimiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itapitiwa.

Mbali na Mwenyekiti Ngicho na Kanali Mntenjele, viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni Mbunge wa Tarime Vijijii, Mwita Waitara, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages