NEWS

Sunday 9 April 2023

Mshauri wa Baraza la Kimila Nyanungu: Hatutaki malumbano na Serikali


Mzee Chacha Mwita Getosi

Na Mara Online News
-----------------------------------

MZEE Mshauri wa Baraza la Kimila Kata Nyanungu katika wilayani Tarime mkoani Mara, Chacha Mwita Getosi amesema hawako tayari kuchonganishwa, au kulumbana na Serikali kuhusu uwekaji wa bikoni (vigingi) kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijii viwili vya kata hiyo; ambavyo ni Kegonga na Nyandage.

Baadala yake mzee huyo ameshauri kuwepo na maridhiano kwa njia ya amani bila malumbano, au vitisho kutoka pande zote.

Aidha, Getosi ambaye ni mmoja wa wazee wa kimila maarufu katani Nyanungu, amekosoa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya chama tawala - CCM, Mwita Waitara na Diwani wa Kata hiyo, Tiboche Richard kijijini Kegonga Aprili 1, 2023, akisema umesababisha wasiwasi kwa wananchi wa vijiji hivyo.

“Tukilaani watoto tunaharibu nchi yetu, wengine ni wasomi na wengine ni wafanyakazi - ni watoto, walikimbia kwenda huko [kusaidia uwekaji wa bikoni] kufanya kibarua kama wanavyofanya Msege [mgodi mdogo wa dhahabu],” mzee Getosi alisema kijijini Nyandage juzi katika mazungumzo maalumu na gazeti la Sauti ya Mara na chombo dada chake cha mtandaoni cha Mara Online News.

Alitoa wito kwa wananchi na viongozi wa Serikali kutambua vijan waliolaaniwa katika mkutano huo ili waweze kuondoa sintofahamu hiyo kwa faida na maendeleo ya vijiji hivyo na taifa kwa ujumla.

“Kile kitendo kilichofanywa na viongozi wetu ni kibaya. Tukilaani watoto tutapata hasara kubwa sana. Tukilaani watoto tunarahibu nchi yetu, ni makosa kabisa,” alisisitiza mzee Getosi na kutamka kuwa hana watoto wa kulaani katika eneo lake la uongozi.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa mmoja wa viongozi hao wa kuchaguliwa aliwashawishi baadhi ya wazee wa kimila kulaani vijana waliokuwa wamepata ajira ya muda ya uwekaji wa bikoni kwenye mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na vijiji hivyo.

Mzee Getosi alisema vijana hao walihitaji kuelemishwa badala ya kuwalaani. Hivyo alioonesha kutoridhishwa na kitendo hicho.

“Sasa kama mbunge aliona kazi ile ni makosa, wangemaliza kuweka bikoni angetuita tukae mkutano, wao waliona kuwa ni kibarua kama vile Msege. Kama ni hivyo tutakuwa tunalumbana na Serikali Kuu, na Serikali ndiyo kubwa, ndio wana maamuzi,” alisisitiza.

Alisema mkutano huo haukuwa wa tija na umeleta taharuki miongoni mwa wananchi wa vijiji hivyo na kuomba Serikali ngazi ya wilaya na mkoa kusaidia kuweka mambo sawa kwa njia ya vikao au mikutano ya pamoja.

“Mpaka sasa watu wengine wanasita sana [wana wasiwasi] hawalali hata ndani ya nyumba. Kumbe hii nchi yangu ya kata ya Nyanungu imeharikiba,” alisema Getosi na kuomba viongozi wa mkoa na wilaya, Mbunge Waitara na Diwani Tiboche kufika Kegonga na Nyandage ili washirikiane na wazee wa kimila, viongozi wa vijiji na vitongoji kumaliza sintofahamu iliyopo katika vijiji hivyo.

“Serikali ya mkoa, wilaya, wananchi na wazee wa mila tukae tutatue matatizo yetu, tuwe pamoja, waache kuchochea. Wanataka tupigane, tukipigana hatuwezi kuwa na maendeleo,” aliongeza mzee Getosi.

Hata hivyo kulingana na vyanzo vyetu vya uhakika, uwekaji wa bikoni katika viiji hivyo umekamila kwa amani na kazi hiyo inaendelea kwenye kata jirani za Gorong’a na Kwihancha; ambapo kumeshuhudiwa ushirikiano mzuri na wataalamu wa Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wanaofanya kazi hiyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages