NEWS

Monday 10 April 2023

Barrick North Mara, wakandarasi wakabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 117 katika Kituo cha Afya Sungusungu


Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (mwenye suti) na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko wakati wa makabidhiano ya msaada wa vifaa tiba katika Kituo cha Afya Sungusungu.

Na Mara Online News
-------------------------------

MGODI wa Dhahabu wa North Mara na wakandarasi wanaofanya nao kazi wamekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 117 katika Kituo cha Afya Sungusungu kilichopo Nyamongo wilayani Tarime.

Kampuni za wakandarasi zilizohusika ni pamoja na Kemanyanki, RES, Wings, Boart Longyear, AKO, PKM na Gokona, miongoni mwa nyingine.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kituoni hapo leo Aprili 10, 2023, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko amesema wameshirikiana na wakandarasi hao kuchanga shilingi milioni 141.857 kwa ajili ya ununuzi na ufungaji wa vifaa hivyo.

Sehemu ya vifaa tiba vilivyotolewa msaada katika Kituo cha Afya Sungusungu

“Desemba 2022 mimi na wafanyakazi wenzangu tulitembelea kituo hiki na kujionea mapungufu ya vifaa tiba. Kwa kuzingatia umuhimu wa kituo hiki katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na wafanyakazi wa mgodi, Januari 2023 niliagiza idara yetu ya Mahusiano na ile ya Afya kuandaa kikao na wakandarasi wanaofanya kazi mgodini ili kwa pamoja tuone namna tunavyoweza kuchangia manunuzi wa vifaa tiba,” amesema GM Lyambiko.

Amesema vifaa hivyo vitasaidia kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya zikiwemo za mama na mtoto katika kituo hicho, na kwamba msaada huo ni sehemu ya uwajibikaji wa mgodi wa North Mara na wakandarasi hao kwa jamii inayouzunguka.

“Malengo ya mgodi ni kuendelea kushirikiana na wakandarasi wote kama wadau muhimu katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka ili kuimarisha mahusiano na mshikamano,” amesema GM Lyambiko.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto) akisaini makabidhiano ya vifaa hivyo. Kulia ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.
Mbunge Waitara akisaini makabidhiano ya vifaa hivyo

Akipokea na kukabidhi vifaa tiba hivyo kwa uongozi wa Kituo cha Afya Sungusungu na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameushukuru mgodi wa North Mara na wakandarasi hao, akisema wameweka alama nzuri katika eneo hilo.

“Haya yote ni matunda ya mahusiano na ushirikishwaji,” amesema Mbunge Waitara na kuahidi kuandika barua ya kuushukuru mgodi na wakandarasi hao kutokana na msaada huo wa vifaa tiba.

Mbunge Waitara ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wadau hao wa maendeleo kuangalia uwezekano kutoa msaada wa ujenzi wa majengo ya huduma za upasuaji na za mama na mtoto katika kituo hicho.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Sylvanus Gwiboha ameshukuru na kusema msaada huo una maama kubwa katika utoaji wa huduma bora za afya.

“Afya bora haiwezi kupatikana kama hakuna vifaa tiba bora. Ninaamini Mungu atawabariki kwa kazi hii nzuri. Vifaa mlivyotoa vitawapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda wilayani kutafuta huduma za vipimo vya afya.

“Kwa msaada huu wa vifaa tiba mmegusa Ilani ya chama tawala - CCM katika kuhakikisha vituo vya afya vinajengwa na kuwezeshwa,” amesema Gwiboha na kuhimiza utunzaji na matumizi sahihi ya vifaa hivyo.


Naye Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Malema Soro amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha mgodi wa North Mara na wadau wote wa maendeleo katika eneo hilo hawabughudhiwi katika utekelezaji wa shughuli zao.

“Viongozi tusimamie wadau hawa wasibughudhiwe katika kazi zao maana wakizalisha zaidi watatoa kitu kikubwa zaidi kwa jamii. Hapa wamemsaidia Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutupatia vifaa tiba ambavyo vinakwenda kusaidia wananchi wetu,” amesema Malema.


Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo ni pamoja na Diwani wa Viti Maalum, Felister Range na wenyeviti wa vijiji, Paul Bageni (Mjini-Kati) na Mwita Msegi (Nyangoto).

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages