NEWS

Wednesday 10 May 2023

CCM Tarime kukutana na wenyeviti waliotangaza kujiuzulu NyanunguNa Mara Online News
------------------------------------

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara wanatarajiwa kukutana na wenyeviti wa vijiji na vitongoji waliotangaza kujiuzulu nyadhifa zao - wakipinga vigingi vya mpaka vilivyowekwa na serikali kutengenisha maeneo yao na Hiafdhi ya Taifa ya Serengeti.

Taarifa kutoka vyanzo vyetu vya uhakika zinasema viongozi hao wa CCM watakutana na wenyeviti hao leo Mei 10, 2023 katika kijiji cha Mangucha ambapo ni makao makuu ya kata Nyanungu.

“Tayari wenyeviti wa vijiji (walioripotiwa kujiuzulu) wamealikwa mkutano huo na tumeambiwa tunakutana na kiongozi mkuu wa CCM Wilaya,” kimedokeza chanzo chetu cha habari kutoka Nyanungu mapema leo asubuhi.

Baadhi ya wenyeviti wa serikali za vijiji na vitongoji katika kata za Nyanungu na Gorong’a waliripotiwa ‘kubwagwa manyanga’ juzi.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa vijiji vya kata ya Nyanungu wamepokea taarifa za kujiuzulu kwa viongozi hao kwa hisia tofauti, wengi wao wakieleza kushangazwa na hatua hiyo.

“Hili suala la viongozi wetu kurudisha mihuri (kujiuzulu) halina maana, mawaziri walifika Nyanungu na tukaona hili suala limeisha lakini kama wamejiuzulu, tuna vijana wengi watashika hatamu,” amesema mmoja wa wazee maarufu kutoka kijiji cha Kegonga katika mazungumzo na Mara Online News kwa njia ya simu.

Mzee huyo amesema wenyeviti hao walitangaza uamuzi huo bila kushirikisha wananchi waliowachagua na kwamba taarifa za kujiuzulu kwao wamezipata kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“Tumeshangazwa sana na huo mchezo wa kujiuzulu. Hivi sasa walijiuzulu wakiwa wapi mbona hata hawakutushirikisha?” amehoji mzee huyo.

Wananchi wengine wamesema viongozi hao walipanga ‘kuachia ngazi’ muda mrefu - endapo vigingi hivyo vingeonekana kumega mashamba na miji ya wananchi.

“Wananchi wengine wanaona ni sawa kwa sababu wameachwa bila mashamba,” amesema mkazi wa kijiji cha Nyandage kwa sharti la kutotajwa jina.

Taarifa zaidi zinasema wenyeviti hao ambao hata hivyo inaelezwa hadi jana jioni walikuwa hawajawasilisha barua za zao za kijiuzulu kwa mamlaka husika, kikiwemo chama chao cha CCM.

Taarifa za kujiuzulu kwa wenyeviti hao wa vijiji na vitongoji zimeripotiwa siku chache baada ya Mawaziri wenye dhamana za TAMISEMI, Ardhi na Maliasili kufika katika kata ya Nyanungu kukutana na wananchi wa eneo hilo na kuwaelimisha uhalali na umuhimu wa mpaka unaowatenganisha na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Katika siku za karibuni, baadhi ya viongozi wa kisiasa ngazi ya kata na vijiji katani Nyanungu wanaotokana na chama tawala - CCM wamekuwa wakitoa kauli za kutishia kujiuzulu nyadhifa zao.

Wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi wamekuwa wakikitupia lawama chama hicho ngazi ya wilaya kwa kukaa kimya bila kuwachukulia hatua viongozi hao kutokana na misimamo yao ya kukinzana na serikali na matakwa ya wananchi walio wengi.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages