NEWS

Monday 10 July 2023

AICT Mara, Right to Play wakazia elimu kwa watoto wa kike



 

Na Joseph Maunya, Tarime
------------------------------------

KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play wamewahimiza wazazi na walezi kuwapa watoto wa kike nafasi ya kupata elimu ili kuwawezesha kufikia ndoto zao na kupambana na umaskini katika familia zao.

Hayo yalisisitizwa na Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota katika tamasha la michezo lililoshirikisha wanafunzi wa shule za msingi Nyamwaga na Maika, walilolianda kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari JK Nyerere iliyopo kata ya Nyamwaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, wiki iliyopita.



Rebeca akizungumza wakati wa tamasha hilo

“Ni muhimu kuwapa watoto wa kike fursa ya kupata elimu iliyo bora na jumuishi, lakini pia kutokatisha ndoto zao za elimu kwa kuwaozesha katika umri mdogo; badala yake waachwe wasome ili baadaye waje kusaidia familia zao kuondokana na umaskini.

“Lakini pia tuwape moyo wa kusoma na siyo tu kuwaandikisha shule na kuwaacha bila kuwapa ushauri juu ya umuhimu wa kupata elimu, jambo linalowafanya wanakata tamaa na kushindwa kuendelea na masomo,” alisisitiza Rebeca.


Afisa Mradi huyo alisema lengo la Shirika la Right to Play ni kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata fursa sawa ya kupata elimu bora na iliyo jumuishi, kutokana na hamasa wanazotoa matamasha ya michezo mbalimbali ambayo pia yanasaidia kujenga na kukuza uwezo wa kitaaluma kwa wanafunzi.

“Katika kukuza ubora wa elimu na iliyo jumuishi, tunatumia michezo na midahalo mbalimbali ambayo siyo tu kwamba inawaburudisha watoto, lakini pia inawasaidia kukuza uwezo wao wa kitaaluma, ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu pale wanapomaliza darasa la Saba,” alisema Rebeca.



 

Kwa mujibu wa Rebeca, Shirika la Right to Play linafanya kazi zake katika kata za Nyamwaga, Itiryo na Nyasincha zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, hususan kuandaa matamasha ya michezo kwa watoto na kusaidia wenye mahitaji maalumu wakiwamo wa kike.

“Sisi kama wasichana tuna haki ya kusoma, hivyo wazazi wawaache watoto wao wa kike wasome maana wanaweza wakawa viongozi wa baadaye kama Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan,” alisema Bina Chacha Magige, mwanafunzi wa darasa la sita kutoka Shule ya Msingi Nyamwaga.

Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwl Gimase Marwa alilishukuru Shirika la Right to Play kwa kuandaa tamasha hilo na kutoa wito wa kuwahimiza wazazi kuwapa nafasi watoto kushiriki matamasha ya michezo ili waweze kujifunza mambo mengi yenye faida kwao na jamii kwa ujumla.  


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages