NEWS

Monday 10 July 2023

Utekelezaji miradi Tarime Vijijini ulivyompa raha Kiongozi wa Mwenge wa UhuruKiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim akikagua mradi wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Na Mwandishi Maalumu

---------------------------------

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara, akisema umezingatia viwango vya ubora na kuaksi thamani ya fedha (value for money) zilizotumika.

Kaim aliyasema hayo wazi katika miradi yote ya maendeleo aliyotembelea, kuikagua, kuizindua na kuiwekea mawe ya msingi ndani ya halmashauri hiyo, Alhamisi iliyopita.

“Tumeona, mwenye macho haambiwi tazama, tumepitia nyaraka zenye taarifa zinazohusiana na miradi, viwango vya ubora vimezingatiwa, miradi inakidhi thamani ya fedha zilizotumika.

“Ninawapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kutokana na namna ambavyo mnatumia vizuri fedha za umma kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwenye hili naomba niwe muwazi, katika utekelezaji wa miradi viwango vya ubora vimezingatiwa.

“Tuendelee kusimamia miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ikamilike kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa,” alisema Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Alieleza kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi.

“Naipongeza kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Jemedari Mama Shupavu, Dktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya, na wana-Tarime tumeona, mwenye macho haambiwi tazama, ni historia, hakika Rais anaupiga mwingi sana,” alisema Kaim.

Idadi ya miradi ya maendeleo iliyotembelewa na Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni saba, yenye thamani ya shilingi bilioni 4.3, kwa Mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji (DED), Solomon Shati.

Miradi hiyo ni ya elimu, maji, afya, barabara, mazingira, vijana na huduma za jamii na uchumi, ikiwa ni miongoni mwa mingi inayotekelezwa katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwaboreshea wananchi huduma za kijamii.


DED Shati (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Mwenge wa Uhuru

Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa”.

Usimamizi wa matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo ulioimarishwa na DED Shati, wasaidizi wake na madiwani chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, unatajwa kuwa ndio umechangia kuiwezesha halmashauri hiyo pia kupata hati safi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages