NA MWANDISHI WETU, Musoma
----------------------------------------------
----------------------------------------------
UONGOZI wa Mbeche Asili Products Group (MAPG) umetoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kujitokeza ‘kukishika mkono’ kikundi hicho katika utengenezaji wa viungo vya chai na matumizi yake, kiweze kutimiza malengo ya kimaendeleo.
“Niwaombe wananchi wa mkoa wa Mara, mikoa jirani na Tanzania kwa ujumla kutuunga mkono, ikiwa ni Pamoja na kutumia viungo vya chai tunavyotengeneza vyenye tiba na lishe asili ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Makamu Mwenyekiti wa MAPG, Frank Peter katika mazungumzo na Sauti ya Mara mjini hapa, wiki iliyopita.
Kikundi hicho chenye makao makuu katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, kinaundwa na wanachuo wabunifu waliosoma katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kilichopo Musoma pia.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa MAPG, Anita Mbeche, kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2020. “Mafanikio ya kikundi hiki tangu kianzishwe ni pamoja na bidhaa tunazotengeneza kuendelea kukubalika kwa wateja/ watumiaji,” alisema.
Matarajio ya kikundi hicho alisema ni kuendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kiwango cha juu, kuwafikia wateja wengi zaidi na kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
“Hivyo wanakikundi tunaomba wadau wa maendeleo na serikali kutuunga mkono kwa hali na mali ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisisitiza Anita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Paschal Mahinyira alikipongeza kikundi hicho kwa ubunifu huo wa kutengeneza viungo vya chai vinavyokubalika katika jamii.
“Hiki kikundi ni wanachuo tuliokuwa nao hapa chuoni, tunawapongeza kwa hatua hii ya kuzalisha chai lishe na chai tiba kwa kutumia mazao ya chakula cha asili kisicho na kemikali yoyote, na bidhaa hizi zimekubalika sana baada ya kuingia sokoni,” alisema Mahinyira. 0764195426
Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment