NEWS

Monday 31 July 2023

Wanandoa waripotiwa kuuawa kikatili na watu ambao hawajajulikana Serengeti
Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------- 

WANANDOA waliotajwa kwa majina ya Ndongo Masalu na Ngire, wameripotiwa kuuawa kwa kukatwa na kuchinjwa na watu ambao hawajajulikana katika kijiji cha Singisi, kata ya Nagusi wilayani Serengeti, Mara. 

  Diwani wa Kata ya Nagusi, Andrea Mapinduzi ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo mchana kwamba mauaji hayo yalitekelezwa saa nane usiku wa kuamkia leo Julai 31, 2023 nyumbani kwa wanandoa hao. 

  “Nilipigiwa simu saa nane usiku nikalazimika kuwahi eneo la tukio… Inaelezwa kwamba walivamiwa na watu wasiojulikana ambao waliwashambulia kwa mapanga hadi kufa… mwanaume alichinjwa kabisa na mke wake yeye alikatwakatwa mabegani. 

  “Kilichoshtua majirani ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja hivi aliyekuwa amelala pamoja na wazazi wake hao - ambaye alisikika akilia sana, ndipo watoto waliokuwa wamelala kwenye nyumba nyingine wakaamka kwenda kuona kulikoni - wakakuta mauaji yameshafanyika,” ameeleza Mapinduzi. 

  Kwa mujibu wa diwani huyo, maofisa wa ulinzi na usalama wa wilaya ya Serengeti walifika eneo la tukio baadaye, na kwamba hadi anazungumza na Mara Online News walikuwa wanaendelea na uchunguzi katika eneo hilo. 

  “Maafisa wa usalama wako hapa wanaendelea na taratibu zao za uchunguzi, na mimi tangu saa nane usiku wa kuamkia leo mpaka sasa hivi [mchana] niko kwenye eneo la tukio ,” amesema Mapinduzi. 

  Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo na hatua zilizochukuliwa. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages