NEWS

Saturday 1 July 2023

Watu 48 wafariki dunia katika ajali ya barabarani Kenya



 

WATU 48 wamethibitishwa kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyotokea kwenye barabara ya makutano ya Londiani nchini Kenya jana Ijumaa jioni.

Lori lililosababisha ajali hiyo halikuwa la nchini Kenya kwani lilikuwa na namba za usajili za Rwanda.

Ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 12:30 jioni baada ya lori hilo kupoteza mwelekeo na kuwagonga wapita njia, wafanyabiashara na mabasi ya abiria - maarufu kwa jina la matatu yaliyokuwa kando ya barabara.

Lori hilo liliyagonga mabasi manne, lori mbili, gari la binafsi na basi lingine kubwa la abiria.

Lori hilo lilikuwa likielekea Kericho kabla ya kushindwa na kuacha njia, na kuwagonga makumi ya wachuuzi waliokuwa wakiendelea na shughuli mbalimbali kando ya barabara kuu ya Nakuru-Kericho.

Waziri wa Uchukuzi, Kipchumba Murkomen ametembelea eneo hilo leo Jumamosi asubuhi, akifuatana na maafisa wengine.

Amesema juhudi za uokoaji zinaendelea zikihusisha maafisa kutoka mashirika mbalimbali ya serikali ya kitaifa na kaunti. “Juhudi za uokoaji zitafuatiwa na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo,” ameongeza.

Walioshuhudia ajali hiyo walisema, dereva wa lori hilo alikuwa akijaribu kukwepa kuligonga basi lililokuwa limeegeshwa barabarani baada ya kuwa na kasoro ya kimitambo kabla ya kushindwa kulimudu.

Watu zaidi ya 60 kufikia sasa wamekimbizwa katika hospitali tofauti za Londiani, Kericho na Nakuru kwa ajili ya matibabu.

Jana jioni, juhudi za uokoaji zilikwama kutokana na mvua kubwa iliyoshuhudiwa katika eneo la tukio.

Kutokana an ajali hiyo, Rais William Ruto jana usiku aliongoza taifa kuomboleza vifo hivyo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

“Nchi inaomboleza pamoja na familia ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Londiani, Kaunti ya Kericho. Inasikitisha kwamba baadhi ya walioaga dunia ni vijana wenye mustakabali mzuri na biashara. watu ambao walikuwa kwenye kazi zao za kila siku.

“Tunawaombea wapone haraka wote walionusurika; mko kwenye mawazo yetu. Tunawaomba madereva wa magari kuwa waangalifu sana barabarani, hasa wakati huu tunapokabiliwa na mvua kubwa,” alisema Rais Ruto. BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages