NEWS

Saturday 11 November 2023

Serikali ya Awamu ya Sita kuunganisha Tarime na Serengeti kwa lami, TANROADS yakabidhi kazi kwa mkandarasi



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (wa nne kushoto), Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe (wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakati wa kumkabidhi mkandarasi barabara ya Tarime Mjini – Mogabiri na Nyamongo – Mugumu/ Serengeti kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, wilayani Tarime jana. (Picha na Sauti ya Mara)
-------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Mara
----------------------------------------

HATIMAYE Serikali imetoa shilingi bilioni 81.146 kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa barabara ya lami kipande cha Tarime Mjini – Mogabiri (km 9.3) na kile cha Nyamongo – Mugumu/ Serengeti (km 51.75) kwa kiwango cha lami.

Hayo yalielezwa na Menaja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe, wakati wa kumkabidhi mkandarasi atakayetekeleza ujenzi huo, mbele ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, mjini hapa jana.

“Serikali tayari imeshapata mkandarasi, imeshasaini mkataba, hivyo TANROADS tumekuja kumkabidhi mkandarasi ili ujenzi uanze,” alisema Mhandisi Maribe.

Alifafanua kuwa ujenzi wa vipande vyote vya Tarime Mjini – Mogabiri na Nyamongo – Mugumu/ Serengeti vyenye urefu wa kilomita 61 utagharimu shilingi bilioni 81.146 kutoka serikalini.

Aidha, Mhandisi Maribe alisema kipande cha Tarime Mjini – Magabiri kitakachojengwa kitakuwa na upana wa mita 9.5, ambapo mita 6.5 ni kwa ajili ya magari na mita 1.5 kila upande ni kwa ajili ya watembea kwa miguu.

“Utekelezaji wa mradi huu utahusisha pia ujenzi wa makaravati na madaraja kadhaa, na utachukua miaka miwili [Novemba 2023 - Novemba 2025] hadi kukamilika,” alibainisha.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, DC Mntenjele aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuikumbuka wilaya ya Tarime kwa miradi ya maendeleo.

Aidha, alimwomba mkandarasi kutimiza wajibu wake kwa kutekeleza ujenzi huo kwa wakati na kwa kiwango walichokubaliana kwenye mkatababa, ili kukidhi thamani ya fedha na matarajio ya Serikali.

“Rai yangu kwa mkandarasi, mradi huu utekelezwe kwa wakati na kulingana na makubaliano ya kwenye mkataba na si vinginevyo. Kwa kufanya hivyo barabara itadumu na kuleta manufaa kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,” alisisitiza.

DC Mntenjele alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wakazi maeneo ambayo ujenzi huo unafanyika kumpa mkandarasi ushirikiano, ikiwemo kusaidia ulinzi wa vifaa vya ujenzi. “Tusije kuanza kufanya udokozi jambo ambalo litarudisha nyuma mradi na kusababisha usikamilike kwa wakati,” alionya.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Novertus kibaji alimshukuru Rais Samia akisema: “Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime, ninamshukuru sana Rais wetu, lakini pia wabunge wetu kwa kuisukuma Serikali kutekeleza miradi hii, naomba mkandarasi aharakishe ujenzi maana tunahitaji kuona matokeo chanya kwa haraka zaidi.”

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Petro Kurate, mbali na kumshukuru Rais Samia, alisema ujenzi huo utatekelezwa katika mazingira ya amani. “Niwathibitishie wakandarasi kuwa amani ipo na tutawapa ushirikiano,” alisema.

Viongozi hao walisema ujenzi wa barabara hizo ambao utatekelezwa na kampuni ya Kichina ya Steco Corporation Ltd, utakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa wilaya za Tarime na Serengeti mkoani Mara.

“Barabara hii ikikamilika kwa kiwango cha lami kwanza itarahisisha usafiri wa abiria na bidhaa mbalimbali yakiwemo mazao ya kilimo kati ya mji wa Tarime na Mugumu, Serengeti, lakini pia itachochea ukuaji wa sekta ya utalii, ikizingatiwa kuwa wilaya hizi zinapakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti,” alisema DC Mntenjele.

Pia, ujenzi wa vipande hivyo vya barabara kwa kiwango cha lami utatengeneza ajira kwa vijana, sambamba na fursa za biashara ndogo ndogo zikiwemo za mama lishe, na hivyo kuwaongezea wananchi kipato.

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages