NEWS

Saturday 11 November 2023

Kahawa ya Tarime yazidi kutamba kwa ubora ndani na nje ya nchi, yashika nafasi ya pili kitaifa



Kahawa kavu aina ya Arabica inayozalishwa wilayani Tarime

NA MWANDISHI WETU, Musoma
--------------------------------------------


KAHAWA inayozalishwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, imeendelea kutamba kwa ubora, ambapo safari hii imeshika nafasi ya pili kitaifa, ikitanguliwa na ya Arusha.

Ushindi huo ulitangazwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) iliyoendesha mashindano yaliyofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro, Oktoba 29, 2023.

Wilaya ya Tarime imewahi kushinda tuzo hiyo ya kahawa bora mara mbili mfululizo, kabla ya ushindi huo wa kushika nafasi ya pili mwaka huu.

Meneja Mkuu (GM) wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd), Samwel Marwa Gisiboye, aliwambia waandishi wa habari mjini Musoma jana Alhamisi kwamba ushindi huo ni fahari kubwa kwa wakulima husika wa zao hilo la biashara.

Itakumbukwa kwamba WAMACU Ltd iliibuka mshindi wa Tuzo ya Chama Bora cha Ushirika katika Usambazaji wa Mbolea Kanda ya Ziwa.

Tuzo hiyo ilitoletwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, yaliyofanyika kitaifa mkoani Tabora, Oktoba 13, 2023.

WAMACU Ltd ni miongoni mwa Vyama Vikuu vya Ushirika vilivyopewa dhamana ya kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima, kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP.

Chama hicho kinajishughulisha na ukusanyaji wa kahawa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuiongezea thamani na kuitafutia masoko ya nje. Pia kwa sasa kina leseni ya kusambaza pembejeo kutoka TISCI, pamoja na leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka TFRA.

Wilaya ya Tarime imejaaliwa ardhi inayostawisha kahawa, hususan aina ya Arabica, inayotamba pia katika soko la dunia.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa soko la kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime ni kubwa, hali inayoifanya kuwa bidhaa adhimu kwenye soko la dunia, hususan katika mabara ya Ulaya, Amerika na Asia.

Kahawa hiyo inaelezwa kuwa na ladha halisi (natural taste) kutokana na sababu zinazotajwa na watalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

Sababu kuu zinatajwa kuwa ni matumizi madogo ya viuatilifu na mbolea za viwandani, ambapo inakadiriwa kuwa katika wakulima 10 wa kahawa wilayani Tarime, ni wawili wanaotumia viuatilifu.

Lakini pia mfumo mzuri wa uzalishaji na uchakataji wa kahawa ya Arabica wilayani Tarime, unachangia ubora na ladha halisi yenye virutubisho vinaotakiwa katika soko la dunia.

“Tarime ina udongo wa volcano na misimu miwili ya mvua; vyote hivi vinaifanya kuwa sehemu sahihi ya kilimo cha kahawa aina ya Arabica,” anasema Mkaguzi wa Kahawa Wilaya ya Tarime, Stanley Rubalila.

Hivyo kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime imeendelea kuwa na soko kubwa katika mataifa yaliondelea duniani, ikiwemo Marekani na Uingereza, ingawa hata hivyo uzalishaji wake bado ni mdogo usiokidhi mahitaji ya soko.

WAMACU Ltd imepata leseni ya kuuza kahawa moja kwa moja katika soko la dunia, baada ya kuikusanya kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Msingi na Ushirika (AMCOS), ambapo inaiuza katika masoko ya nje ya Tanzania kama vile Uingereza na Marekani.

Pia kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime inauzika vizuri katika nchi za Uholanzi, Ugiriki, Uhispania, Ujerumani, Costa Rica na Colombia.

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli wa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages