NEWS

Tuesday 27 February 2024

Mweka Hazina Serengeti alivyokutana na moto wa Majaliwa, atiwa mbaroni kwa ‘upigaji’ wa milioni 213/-



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa 
akizungumza wilayani Serengeti jana.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
------------------------------------------


MKUU wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Saad Mutunzi Ishabailu amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya Waziri Mkuu, Kassim majaliwa kutokana na kosa la kushiriki kuhujumu shilingi milioni 213.7 za umma.

Ishabailu anadaiwa kuhamisha kiasi hicho cha fedha kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani kwa kushirikiana na watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi, alitoa agizo la kukamatwa kwa Ishabailu jana jioni wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika kikao kilichofanyika mjini Mugumu.

“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP aelezwe afungue jalada la mashtaka. Wale wenzake tumewapeleka mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana,” alisema Majaliwa.

Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali alifikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza watumishi na madiwani mbinu wanazotumia watumishi wachache wa baadhi ya halmashauri, ambao wamekuwa wakishirikiana na watumishi watatu wa kitengo cha Treasury Single Account (TSA) kuiba fedha za umma.

Alifafanua kuwa Ishabailu alishiriki kupiga fedha hizo za umma kisiri bila Mkurugenzi, Mwenyekiti, Afisa Mipango na wakuu wa idara nyingine wa halmashauri hiyo kujua.

Akitolea mfano mbinu zinazotumika na wachache hao, Waziri Mkuu alisema Juni 10, 2023 walitumia mwanya wa kuombea kibali fedha za bakaa kwa barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Chatta Luleka kwenda HAZINA.

“Nilituma timu yangu hapa ije kufanya uchunguzi, ikawahoji baadhi ya watumishi akiwemo Afisa Mipango wa Halmashauri, Bw. Wilfred Mwita ambaye alisema hajui uwepo wa hizo fedha, wala hawakuwa na mpango wala bajeti inayohitaji hizo fedha. Mkurugenzi wa sasa, Bw. Furaha alipoulizwa naye alisema hajui uwepo wa hizo fedha, kwani alianza kazi Agosti, mwaka jana.”

Majaliwa alisema Juni 21, mwaka jana Ishabailu alianza kufanya matumizi ya hizo fedha kwa kushirikiana na mfanyabiashara wa mjini Mugumu, Daudi Matinde Chacha kupitia kwenye akaunti zake za NMB na CRDB kwa kupitia miamala minne ya shilingi milioni 76.3, milioni 57.7, milioni 47 na milioni 32.5.

Alisema Matinde alipoulizwa na timu ya uchunguzi alikiri kuwa hadai fedha yoyote Halmashauri ya Serengeti isipokuwa Mweka Hazina huyo aliomba apitishie fedha zake kwenye akaunti zake kwa sababu zinahitajika haraka kwa matumizi ya ofisi.

“Aliambiwa atoe shilingi milioni 189 akamkabidhi zote Bw. Ishabailu na zilizobakia (milioni 24) akaambiwa abaki nazo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa na kuendelea:

“Baada ya kupokea fedha hizo, Bw. Ishabailu alipanda basi kutoka Serengeti hadi kituo cha mabasi Nyegezi, Mwanza na kumkabidhi Bw. Zablon Mponzi ambaye alisema zinatakiwa haraka na wakubwa huko Dodoma, bila kuwataja wakubwa hao ni akina nani. Yeye pia alikabidhi shilingi milioni 150 kwa huyo Zablon, ina maana alibakia na shilingi milioni 39.”

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwasisitiza madiwani na watumishi kuwa makini na matumizi ya fedha za umma kwani Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anapozitafuta na kuzipeleka kwenye halmashauri anataka zisaidie kutatua kero za wananchi.

Leo Jumatano, Waziri Mkuu anaenelea na ziara yake ya kikazi kwa siku ya nne mkoani Mara, ambapo atakagua miradi ya maendeleo na kuhutubia mikutano ya hadhara katika wilaya za Rorya na Tarime.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages