Baadhi ya mbuzi na kondoo waliouawa na chui kijijini Robanda.
-------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
--------------------------------------------
KATIKA tukio lisilo la kawaida, mnyamapori aina ya chui ameripotiwa kuvamia na kuua mbuzi na kodoo 34 kwa wakati mmoja usiku katika kijiji cha Robanda wilayani Serengeti, Mara.
Tukio hilo linatajwa kuwa la kihistoria na la kwanza kwa mnyamapori kuua idadi kubwa ya mifugo kwa wakati mmoja kijijini hapo.
Hata hivyo, hajabainishwa iwapo chui huyo alitoka kwenye Mapori ya Akiba Ikorongo na Grumeti, au Hifadhi ya Taifa Serengeti kwani kijiji cha Robanda kinazungukwa na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji cha Robanda, Mrobanda Japan alikiambia chombo cha habari kwamba chui huyo aliua mifugo hiyo kwa kuivunja shingo na kuinyonya damu majira ya saa mbili usiku wa kuamkia Machi 16, mwaka huu.
“Ni tukio ambalo kwa kweli linahuzunisha kwa sababu yamekuwa yakitokea matukio mengi ya mifugo kuuawa kwa idadi ndogo kama tano, sita, saba, nane lakini hili ni la kwanza kwa kuua mifugo mingi kwa wakati mmoja katika kijiji changu,” alisema Mrobanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti.
Mmiliki wa mifugo iliyouawa na chui katika tukio hilo la kihistoria, Machage alisema alikuwa kazini nje ya nyumbani kwake wakati mkasa huo unatokea.
“Nilikuwa kazini, nyumbani alikuwa mke wangu, na taarifa niilipata asubuhi kuwa minfugo imeisha, nilipokwenda nikakuta kweli nilichokichuma kimeisha chote,” alisema Machage.
Akizungumzia tukio hilo, Mhifadhi Daraja la Kwanza na Mwikolojia wa Mapori ya Akiba Ikorongo na Grumeti, Lasco Francis Chuwa alisema ni vigumu kwa kijiji cha Robanda kuepuka matukio ya mifugo kuuawa na wanyamapori wakali kutokana na kuzungukwa na maeneo ya uhifadhi.
“Kijiji cha Robanda kinapakana na hifadhi pande zote, hivyo kipindi kama hiki tunapata tatizo kubwa la hawa wanyama wanaokula nyama (carnivals) kwa sababu tunakuwa tumetoka kwenye mvua nyingi ambazo zinasababisha majani yanaota yanakuwa marefu, kwa hiyo wanyamapori wengi ambao wanakula majani wanahama na wanakuwa kwenye makundi madogo madogo.
“Kwa hao wanyama wanaokula nyama inawawia vigumu sana kuwinda, hivyo inabidi watafute vijiji vya karibu ambapo wanajua wanaweza wakapata nyama au chakula kwa urahisi.
“Kwa hiyo chui wanavutiwa kuja kwenye maeneo ya vijiji, na bahati mbaya ni kwamba maeneo mengi ya malisho yana vichaka vingi ambavyo vinasaidia hawa chui kupata maeneo ya kujificha kwa muda mrefu. Kwa hiyo ndiyo maana katika kipindi hiki tunakuwa na shida kubwa ya hawa wanyama wanaokula nyama, hasa chui, simba na fisi,” alisema Mhifadhi Chuwa.
Hata hivyo, taarifa njema ni kwamba tayari chui aliyeua mifugo hiyo ameshakamatwa na kuhamishiwa eneo la mbali.
“Katika operesheni ya kumsaka chui aliyehusika, tulifuatilia nyendo zake na kugundua maeneo anayolala, tukaweka kizimba cha mtego, saa mbili usiku akaingia na kunasa, tukamchoma dawa ya usikinzi kisha tukamsafirisha kwenda kumhifadhi maeneo ya mbali ambayo ni salama kwake na wananchi,” alisema mhifadhi mwingine.
“Tunajitahidi sana hasa kwa hawa wanayama jamii ya paka ambao wengi wako kwenye hatari ya kutoweka, hatupendi tuwaue kwa sababu wamesababisha madhara, tunajitahidi kuwakamata na kuwapeleka maeneo mengine. Mfano huyo chui tumempeleka maeneo ya mbali zaidi ambako ataweza kuishi vizuri na kutoleta madhara kwa wananchi,” alisema Mhifadhi Chuwa.
No comments:
Post a Comment