NEWS

Saturday 23 March 2024

Wanafunzi waishukuru AICT, Right to Play kwa kuwawezesha kutambua haki zaoWanafunzi wakionesha makombe waliyoshinda katika tamasha la michezo yao lililoandaliwa na Right to Play kwa kushirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Keisangora wilayani Tarime jana.
------------------------------------------------

Na Joseph Maunya, Tarime
--------------------------------------


WANAFUNZI wa shule za msingi Keisangora na Nyamirema katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, wamelishukuru Shirika la Right to Play na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, kwa kuwawezesha kutambua umuhimu wa kupata haki yao ya elimu, hasa kwa watoto wa kike.

Walitoa shukrani hizo jana Machi 22, 2024 waliposhiriki tamasha la michezo la uhamasishaji juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, lililoandaliwa na Right to Play kwa kushirikiana na kanisa hilo katika viwanja vya Shule ya Msingi Keisangora.


Shindano la kukimbia.
---------------------------------

“Naishukuru Right to Play kwa sababu kupitia wao nimejua kuwa ni muhimu sana kupata haki ya elimu kwa sisi watoto wa kike, hivyo jamii nzima itusaidie kufikia malengo yetu,” alisema mwanafunzi Janneth Ryoba wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Keisangora.

“Kupitia Right to Play nimejifunza kwamba hawa dada zetu pia wanatakiwa kupata haki ya elimu kama sisi wavulana ili nao wapate nafasi ya kuleta maendeleo katika jamii kupitia elimu watakayoipata,” alisema mwanafunzi Amos John Kisiri wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Nyamirema.


Wanafunzi wakiimba shairi 
wakati wa tamasha hilo.
-------------------------------------------

Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo aliwaomba wadau mbalimbali waliofika katika tamasha hilo kueneza ujumbe walioupata kutoka AICT na Right to Play ili kusaidia kuhamasisha jamii yote kushiriki kuwaondolea watoto wa kike changamoto zinazowazuia kuendelea na masomo.

“Kila aliyefika mahala hapa apeleke elimu kwa jamii kwamba mtoto wa kike apate elimu, asiolewe katika umri mdogo na pia asifanyiwe mambo yanayoashiria unyanyasaji wa kijinsia ili huko mbeleni aweze kupata fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yake na jamii kiujumla,” alisema Fungo.


Fungo akizungumza katika tamasha hilo.
------------------------------------------------

Shirika la Kimataifa la Right to Play limekuwa likishirikiana na AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kuendesha mradi wa kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kupitia matamasha ya michezo na midahalo katika shule mbalimbali za msingi zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages