NEWS

Thursday 11 July 2024

NGO ya Bunda yapokea msaada wa Dola 10,000 kutoka Taasisi ya Rais wa BarrickMeneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (wa pili kulia) akimkabidhi Mwakilishi wa Taasisi ya MWC, Grace Mutoni msaada wa Dola 10,000 zilizotolewa na Taasisi ya NVeP, katika hafla iliyofanyika mgodini hapo mapema leo Julai 11, 2024.
---------------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu, Tarime
------------------------------------------

Taasisi ya Mara Women and Children (MWCF) iliyopo wilaya ya Bunda mkoani Mara imepokea msaada wa Dola za Kimarekani 10,000 (sawa na Shilingi za Kitanzania zaidi ya milioni 26) kutoka Taasisi ya Nos Vies en Partage (NVeP) iliyoanzishwa na Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni Barrick Gold, Dkt Mark Bristow.

Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Apolinary Lyambiko amekabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha kwa Mwakilishi wa MWCF, Grace Mutoni, katika hafla fupi iliyofanyika mgodini hapo mapema leo Julai 11, 2024.

“Tunayo furaha kukabidhi msaada huu wa Dola 10,000 kwa Taasisi ya Mara Women and Children ili kuwezesha wanawake na watoto mkoani Mara, ikiwemo kuwezesha biashara ndogo zinazomilikiwa na wanawake.

“Ni matumaini yetu kuwa huu msaada utatumika kwa lengo lililokusudiwa na hivyo kuchangia kubadilisha maisha ya walengwa wa mradi huu,” amesema GM Lyambiko wakati wa makabidhiano hayo.

Kwa mujibu wa GM huyo, Taasisi ya NVeP inasaidia mashirika manne nchini Tanzania [mawili ya ngazi ya taifa na mawili ya ngazi ya mkoa] kila robo ya mwaka, ambapo kila shirika hupewa Dola 10,000 ili kusaidia makundi ya wanawake na watoto wenye mahitaji maalumu.

Katika hatua nyingine, GM Lyambiko amesema Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unawajibika kujenga jamii endelevu na kuhakikisha unakuwa na uhusiano mzuri na jamii inayouzunguka.

“Kila mwaka mgodi huu unatenga Dola sita kwa kila wakia (ounce) ya dhahabu iliyouzwa na mgodi na kuzielekeza kwenye utekelezaji wa miradi ya kijamii,” amebainisha GM huyo.

Amesema mgodi huo umeshatumia shilingi bilioni 22 kugharimia utekelezaji wa miradi 253 katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo wa Dola 10,000, Mwakilishi wa Taasisi ya MWC, Grace Mutoni amelishukuru Taasisi ya NVeP kupitia mgodi huo na kuahidi kuutumia vizuri ili kugusa makundi ya wanawake na watoto wenye uhitaji mkoani Mara.

“Tumefurahi sana, na kama taasisi tutatumia msaada huu kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuwafikia wanawake na watoto wengi zaidi ndani na nje ya wilaya Bunda,” amesema Mutoni.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages