NEWS

Wednesday, 30 April 2025

Ushirika wa WAMACU wamshukuru Rais Samia uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.
---------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimemshukuru na kumpongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, kutokana na serikali yake kufanikisha uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank).

Kimesema hatua hiyo ni ya kihistoria - ambayo sasa inaweka msingi mpya wa matumaini ya utatuzi wa changamoto za wakulima kote nchini.

Rais Samia alizindua benki hiyo jana Aprili 28, 2025 jijini Dodoma, katika hafla iliyovutia hisia za wakulima nchini, wakiwemo wana-Ushirika wa WAMACU - ambao walifuatilia tukio hilo mbashara kupitia runinga wakiwa katika ukumbi wa kiwanda cha kuchakata kahawa cha ushirika huo mjini Tarime, mkoani Mara.
Wana-Ushirika wa WAMACU wakifuatilia tukio mbashara uzinduzi wa Benki ya Ushirika Tanzania kupitia runinga wakiwa katika ukumbi wa kiwanda cha kuchakata kahawa cha ushirika huo mjini Tarime, mkoani Mara juzi. (Picha na Mara Online News)
----------------------------------------

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa benki hiyo, Rais Samia aliitaka benki hiyo kupanua mtandao wake ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa waishio vijijini.

Alisema uanzishwaji wa benki hiyo si suala la bahati mbaya bali ni wazo la muda mrefu ili kuhakikisha wana-ushirika wanapata mitaji nafuu ili kuendeleza harakati zao za maendeleo.

Aliongeza kuwa benki hiyo ambayo imeanza na mtaji wa shilingi bilioni 58, ni kielelezo cha zama hizi ambazo zinatawaliwa na uchumi wa kisasa jumuishi ambao lengo lake ni kuwashirikisha wananchi wengi zaidi katika kutoa mchango wao kwa uchumi wa taifa lao.

Rais Samia aliwataka watendaji wa chombo hicho kujipanga ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo ubunifu wa kuwajumuisha wananchi wengi katika mkondo mzima wa uzalishaji wenye tija.

Benki hiyo imeanza na matawi manne nchini na imedhamiria kuwa na maelfu ya wateja wakiongozwa na vyama vya ushirika.

Aidha, benki hiyo inatarajiwa kuongeza mitaji kwa wakulima ili shughuli zao za kilimo ziweze kuwa na tija kwa manufaa na ustawi wao na taifa kwa ujumla.

Rais Samia alitumia nafasi hiyo pia kumpongeza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Katibu Mkuu wake, Gerald Mweli, kwa kuwa wabunifu katika wizara yao hadi kufanikisha kuanzishwa kwa benki hito ili kusukuma gurudumu la maendeleo.

Kwa mujibu wa Waziri Bashe, Benki ya Ushirika Tanzania itaongozwa na misingi ya kibiashara ili kuleta tija kwa wateja wake katika zama hizi za uchumi wa soko na maendeleo ya haraka ya teknolojia.

WAMACU walivyofunguka
Wakizungumza na Mara Online News muda mfupi baada ya uzinduzi wa benki hiyo, wajumbe wa Bodi ya WAMACU Ltd, akiwemo Elias Marwa Samwel, walisema Rais Samia ameleta suluhisho la wakulima lililosubiriwa kwa miaka mingi.

"Zamani wakulima walikuwa wanapeleka mazao ghalani, wanapewa stakabadhi bila kupata hela. Wengine walikufa wakisubiri malipo yao. Kupitia COOP Bank, tunaamini matatizo ya wakulima sasa yatabaki historia," alisema Marwa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, Emmanuel Ndege Benson, alisema wakulima wote nchini wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa moyo wa dhati kutokana na msukumo wake uliofanikisha uanzishaji wa benki hiyo.

"Tunamshukuru sana Rais Samia, Benki ya Ushirika inaenda kuleta chachu kwa wakulima, hasa wadogo wadogo ambao walisahaulika - hawakuweza kukopesheka. Mkulima ulikuwa ukifika benki unaambiwa hakuna fursa ya kukopa. Tumefurahi sana kupata benki hii," alisema Ndege.

Mhazini wa WAMACU Ltd, Mohamed Sakiru.
--------------------------------------

Mhazini wa WAMACU Ltd, Mohamed Sakiru, naye hakusita kueleza matumaini yake juu ya benki hiyo katika suala zima la kuimarisha ushirika na kustawisha uchumi wa wakulima nchini.

"Rais katika hotuba yake amezungumzia vitu vingi, kwa uzinduzi huu wa benki yetu ya ushirika nina imani itatuletea mafanikio makubwa katika sekta ya ushirika nchini," alisema Sakiru.

Sakiru alitolea mfano akaunti ya ‘Mkulima Tija’ akisema ni huduma iliyobuniwa kwa kumpendelea mkulima moja kwa moja – ambayo haina makato kwa mkulima na kwamba mikopo yake ni rahisi.

Kwa ujumla, wana-Ushirika wa WAMACU Ltd wameonesha imani kubwa kwa benki hiyo mpya - kwamba si tu itarahisisha upatikanaji wa mikopo, bali pia itachochea uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa tija na kuimarisha sekta ya ushirika nchini.

Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye.
----------------------------------------

Ushirika wa WAMACU Ltd una leseni ya kuuza kahawa nje ya nchi kama vile Uingereza na Marekani, baada ya kuikusanya kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Msingi vya Masoko na Ushirika (AMCOS) na kuiongezea thamani.

Kahawa ya Arabica inayolimwa wilayani Tarime inauzika vizuri katika nchi za Uholanzi, Ugiriki, Uhispania, Ujerumani, Costa Rica na Colombia.

Pia, WAMACU Ltd ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika vilivyopewa dhamana ya kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP.

Aidha, kwa sasa ushirika huo una leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

Oktoba 2023, WAMACU Ltd waliibuka mshindi wa Tuzo ya Chama Bora cha Ushirika katika Usambazaji wa Mbobelea Kanda ya Ziwa - iliyotolewa na TFRA wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Tabora.

Moja ya siri za mafanikio ya WAMACU Ltd ni uwezesho mkubwa ambao imekuwa ikiupata kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa mujibu wa Meneka Mkuu wa ushirika huo, Samwel Marwa Gisiboye.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages