
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma jana Juni 27, 2025. (Picha na Ikulu)
----------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alihitimisha rasmi shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana Juni 27, 2025 jijini Dodoma kwa hotuba iliyojaa mafanikio ya kisekta kutokana na utendaji na uwajibikaji thabiti wa Serikali yake ya Awamu ya Sita.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi, akieleza mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na jinsi ustawi wa wananchi ulivyoimarishwa kupitia sera, mipango na miradi ya Serikali tangu mwaka 2021.
Alisema kipindi cha tangu mwaka 2021 hadi sasa kimekuwa cha kufanya mageuzi makubwa, kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi na kujenga msingi imara wa ukuaji endelevu wenye kasi zaidi na unaowainua wananchi kiuchumi.
Aidha, alisema kimekuwa kipindi cha kuimarisha ustahimilivu wa jamii, kukuza ustawi wa wananchi na kuwawezesha ili kujiletea maendeleo. Halikadhalika, alieleza kuwa uchumi umekua kutoka wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2021 hadi asilimia 5.5 mwaka 2024 na unatarajiwa kufikia asilimia 6 mwaka 2025.
Miongoni mwa mafanikio ya kisekta aliyoyataja ni kuanza kwa treni ya mizigo ya SGR, kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la John Pombe Magufuli “Kigongo-Busisi), uboreshaji wa viwanja vya ndege na ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya usafiri wa majini.
Kuhusu Deni la Taifa, Rais Samia alisema ongezeko lake limechangiwa na kuiva (kulipwa) kwa madeni ya nyuma, kupanda kwa riba kimataifa, tofauti za viwango vya ubadilishaji fedha na uamuzi wa Serikali kutambua madeni ya kabla ya mwaka 1999 ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuilinda na kuwezesha wastaafu kulipwa pensheni.
Aidha, Rais Dkt. Samia alisema serikali yake imeweza kufungua zaidi milango ya uwekezaji ili kuongeza ajira na kupingiza umaskini nchini.
Kuhusu hali ya uchumi, alisema kazi haikuwa rahisi lakini serikali ilichukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwenye kilimo, Rais Samia alisema serikali imeweza kuongezeka bajeti ya sekta hiyo kwa asilimia kubwa kwa lengo la kuongeza tija na kuwezesha nchi kujitosheleza kwa changula.
“Tutaendelea kuimarisha ukosanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada kutoka nje ya nchi kugharimia bajeti yetu,” amesema Rais Samia na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi inayotekelezwa kutokana na fedha za mikopo ili iwe yenye tija kwa nchi.
Vilevile, Rais Samia alisema licha ya kupungua kwa baadhi ya misaada ya kimataifa, Serikali itahakikisha shughuli za kijamii, hasa katika sekta ya afya ikiwemo mapambano dhidi ya UKIMWI haziathiriki na kusisitiza kuwa afya za Watanzania zitaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alimpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa uongozi wake mahiri uliowezesha kufanyika kwa mikutano 19 ya Bunge hilo na kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).
Vilevile, aliwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika kipindi chote cha uongozi wake.
Rais Dkt. Samia alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa Watanzania kuendeleza amani na mshikamano wakati wote, hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, akisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa mafanikio ya pamoja kama Taifa.
Pia, alisema maridhiano na mashauriano ya kisiasa yamechochea mageuzi makubwa ikiwemo urejeshaji wa mikutano ya hadhara, kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kufutwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa vinavyostahili.
Aidha, Rais Samia alisema Serikali itaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Maridhiano, ikiwemo kuanza upya kwa mchakato wa Katiba Mpya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Alitoa rai kwa vyama vya siasa kuwateua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Rais Dkt. Samia alihitimisha shughuli za Bunge la 12 na kutangaza kuwa Bunge litavunjwa rasmi Agosti 3, 2025, hatua inayowezesha kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment