
Pichani ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles (katikati aliyevaa koti), akiwa na madiwani na wadau wengine baada ya harambee ya kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa Kanisa Katoliki Kitenga jana, ambapo alimwakilisha Nyambari Nyangwine kama mgeni rasmi.
--------------------------------------------
Na Godfrey Marwa, Tarime
Kada wa Chama Cha Mapunduzi (CCM) aliyewahi kuwa Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, jana alichangisha harambee na kufanikisha kupatikana kwa shilingi milioni 11.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kanisa Katoliki Kigango cha Kitenga katika kata ya Bumera, wilayani Tarime.
Nyangwine ambaye aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles, kama mgeni rasmi katika harambee hiyo, yeye binafsi alichangia fedha taslimu shilingi milioni tano, huku akiungwa mkono na madiwani zaidi ya 20 na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya kata.
Akizungumza katika harambee hiyo, Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga, alimpongeza Nyangwine kwa moyo wake wa kujitolea kuchangia maendeleo ya dini na jamii kwa jumla.
"Nyangwine anapenda sana kuchangia makanisa, ni mdau wa maendeleo, ni mtu wa kujitolea sana, ndio maana tunampenda. Unapotoa Mungu anakubariki,” alisema.
Aliongeza: "Tunafundishwa upendo kwa kila mtu, sisi tupendane kama unavyojipenda vyote tukivyo navyo ni mali ya bwana.Mungu anatupenda inabidi tumpende zaidi, Nyambari ni rafiki yangu, naye pia ni mtia nia kupitia CCM, akija tumuunge mkono akatuwakilishe bungeni.”

Kiles akimkabidhi Paroko Innocent Mwesigwa kiasi hicho cha fedha.
-------------------------------------
Kwa upande wake kiongozi wa kiroho wa eneo hilo, Paroko Innocent Mwesigwa, alimshukuru Nyangwine akisema: "Nina furaha kubwa sana, mmetuinua Kitenga.”
Paroko Mwesigwa aliongeza: "Mmetupenda bila kutufahamu Nyambari Nyangwine katupenda bila hata kutufahamu na sisi tutampenda."
Naye Diwani wa Kata ya Bumera, Deogratius Ndege, alisema: "Nyambari ni mdau wa maendeleo wilayani Tarime amewekeza kwenye jamii, anasambaza vitabu, anajenga makanisa Tanzania nzima, ndiye aliyesababisha koo 12 za Tarime kuungana na kuleta amani, ni mtu wa vitendo."
Aidha, Nyangwine kupitia kwa Kiles alitoa fedha taslimu shilingi milioni moja kuchangia ukamilishaji wa jengo la ofisi ya CCM Kata ya Bumera.
Muonekano wa sasa wa jengo la Kanisa Katoliki Kigango cha Kitenga.

No comments:
Post a Comment