Mganga mkuu wa Halmashauri
ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Dkt Judith Ringia, amesema wananchi wote watakaohitaji
huduma katika hospitali ya halmashuari hiyo (Somanda) watatakiwa kuvaa barakoa
kama moja ya hatua za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) kuanzia wiki ijayo.
Aidha, Dkt Ringia amesema
kila mwananchi atapimwa joto la mwili kabla ya kuingia na kutoka
hospitalini na kwamba watoa huduma wote watakuwa vifaa kinga.
Dkt Ringia amesema hayo
jana Aprili 21, 2020 mara baada ya uzinduzi wa kutembelea na kutoa elimu katika
maeneo ya mikusanyiko juu ya kujikinga na virusi vya corona vinavyosababisha
homa kali ya mapafu.
DC Kiswaga na viongozi wengine wakitoa elimu ya kujikinga na Covid 19 kwa wananchi |
“Tumeweka mazingira salama
kwa watumishi wetu, ambapo kwa sasa kila mtumishi anavaa barakoa na wao
tunawapima joto la mwili kabla ya kuingia na kutoka ndani ya hospitali,
pamoja na hayo, tutatembelea maeneo yote ya minada, magulio, masoko na
stendi za mabasi na tayari kikosi maalumu kimeundwa kwa ajili ya kutoa
elimu hiyo,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya
hiyo, Festo Kiswaga, ambaye ni mwenyekiti wa timu hiyo, amewataka wananchi
wanaokwenda kutafuta mahitaji kwenye minada, magulio na sokoni kuhakikisha
wanachukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono.
Sambamba na hilo, Kiswaga
amewataka wafanyabishara kuhakikisha wanaweka ndoo ya maji tiririka na sabuni
katika maeneo ya biashara zao na kwamba wananchi wanatakiwa kununua bidhaa na
kuondoka mara moja.
(Habari na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment