NEWS

Tuesday, 16 June 2026

Siku ya Mtoto wa Afrika: MVIWANYA waiadhimisha kwa kupanda miti zaidi ya 750 Rorya, Tarime



Wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi Odikwa wakishiriki kupanda miti iliyopelekwa na MVIWANYA shuleni hapo leo Juni 16, 2026, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kupanda miti.

Na Godfrey Marwa
Rorya
-----------

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima na Wafugaji Nyancha (MVIWANYA) mkoani Mara, chini ya ufadhili wa Vi Agroforestry, wameadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kupanda miti zaidi ya 750 katika wilaya za Rorya na Tarime.

Shughuli hiyo ilianza jana ambapo MVIWANYA walipanda miti katika mashamba ya wakulima katika kata ya Nyakonga wilayani Tarime na kuhitimishwa leo Juni 16, 2026 kwa kupanda miti katika Shule ya Awali na Msingi ya Odikwa wilayani Rorya.

Mkurugenzi wa shule hiyo yenye mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, Jacob Nguka Ogola, ameishukuru MVIWANYA kwa kuendelea kusaidia uhifadhi wa mazingira kwa elimu na vitendo.

"Tunawashukuru sana, tunachukuwa hii kama fursa kwetu kwa kufanya kila linalowezekana kuhifadhi mazingira, tunaomba waendelee kutuunga mkono kwenye suala la kuhifadhi mazingira pamoja na wanafunzi kwenda kujifunza kupitia maonesho,” alisema Nguka.

Mkurugenzi Jacob Nguka Ogola

Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo ya Odikwa, Mary Deus Marwa, alisema "Tumeipokea hii Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kujifunza masuala ya haki ya mtoto kuishi na kujifunza katika mazingira bora na salama. Pia kupanda miti na umuhimu wake katika mazingira yetu. Siku hii inaikumbusha jamii kuwapatia watoto malezi bora, kwani malezi bora ni msingi wa taifa la kesho.”

Mwanafunzi Mary Deus Marwa. (Picha zote na Mara Online News)

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika Juni 16 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu wa 2026 inasema “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages