Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe
ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji kwa
ajili ya ujenzi wa Viwanda katika mikoa yao.
Prof. Shemdoe aliyasema hayo Wilayani Kahama alipokuwa
anakabidhiwa eneo la hekari 62 zilizotolewa bila fidia na Halmashauri ya mji ya
Wilaya kahama kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kuanzisha kituo
maalumu cha utafiti (centre of excellency)
kitakachotumiwa na Taasisi za utafiti zilizo chini ya Wizara pamoja na
taasisi nyingine kwa ajili ya utafiti unaolenga kuongeza thamani wa zao la
pamba.
Prof. Shemdoe alisema “nimefarijika kuona namna halmashauri ya mji
Kahama ilivyoweza kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli la
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda, kwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya
uwekezaji.
“Nawashauri Halmashauri nyingine nchini kuja Kahama kujifunza
jinsi Wilaya hii ilivyoweza kuendeleza maeneo hayo yaliotenga ikiwemo uwekaji
wa miundombinu kama vile maji, umeme, bararabara na njia za mawasiliano”.
Prof. Shemdoe alisema eneo hilo walilokabidhiwa, kwa Wizara itajenga
kituo kitakachotumika kuongeza thamani ya zao la Pamba.
“Tunatarajia kujenga kituo maalumu cha kutoa huduma za utafiti kwa
zao la pamba ili mkulima aweze kufaidika na zao hilo kwa kuzingatia mnyororo wa
thamani”.
Awali katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe alitembelea eneo lilotolewa
na Halmashauri kwa mwekezaji mzawa kampuni ya KOM group of Companies ambaye
amejenga kiwanda kinachotarajiwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo maji, vinywaji
na vifungashio.
Aidha, Prof. Shemdoe alitembelea eneo la Viwanda vidogo la Zongomela
ambalo Halmashauri ya Wilaya Kahama imetoa kwa wajasiriamali wapatao 1500 wanaozalisha
bidhaa mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa Samani, Mashine za kusagia mawe ya
dhahabu na utengenezaji wa bidhaa za chuma na aluminiamu.
Naye Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack alieleza kuwa
amefarijika kwa kuona Wizara imefika kuona kazi ambayo Halmashauri na Mkoa inafanya.
“Sisi kama Mkoa tulikaa chini na kuona namna ya kutekeleza
maelekezo ya Mhe. Rais ya kuifanya Tanzania kuwa ya Viwanda, hivyo tukaamua
kutekeleza kwa vitendo maagizo hayo”.
Aidha aliwashukuru Mamlaka ya Uendelezaji wa Mauzo ya nje EPZA kwa
ushirikiano walioutoa kwa Halmashauri hiyo
No comments:
Post a Comment