Uongozi
wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Tarafa wa mkoa baada ya
makabidhiano ya Pikipiki zilizotolewa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli.
Katibu
Tawala wa MKoa wa Rukwa Benard Makali akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo bahasha yenye funguo za Pikipiki ili aweze kutoa
Pikipiki kwa Afisa Tarafa (hayupo pichani)kwa niaba ya maafisa tarafa
wenzie.
Pikipiki hizo
zimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa
tarehe 04.06.2019 baada ya kufanya kikao kazi na Maafisa Tarafa wote nchini alipokutana
nao Ikulu Jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika
hafla fupi ya kukabidhi pikipiki hizo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo
alimshukuru Rais kwa kutimiza ahadi hiyo huku akiwasisitiza maafisa hao
kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na Rais ikiwemo kusimamia
mapato, miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao pamoja na kusikiliza kero
za wananchi.
Alieleza kuwa katika
ziara zake alizozifanya katika maeneo ya vijijini, alibaini kuwepo kwa mwamko mdogo
wa wananchi juu ya ugonjwa hatari wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi
vya Corona (Covid-19) hivyo kuwataka maafisa hao kuhakikisha wanavitumia vyombo
hivyo kufikisha elimu ya ugonjwa huo hatari.
“Ni Imani
yangu kuwa tutavitumia vyombo hivi vya usafiri kuhakikisha kuwa tunawafikia
wananchi wetu kwenye maeneo yao ili tuweze kuwahamasisha kujikinga na ugonjwa
huu hatari ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka
mara kwa mara na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,” Alisema
Aidha, Alimtaka Katibu
Tawala wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anachukua hatua kali za kisheria na
kiutumishi kwa Afisa Tarafa yeyote atakayetumia pikipiki hiyo kinyume na malengo
ya serikali ikiwemo kutumia kama Bodaboda na kuongeza kuwa pikipiki hizo zina
namba za serikali, hivyo, kuzitumia kinyume na malengo yake ni ukosefu wa
maadili.
Afisa
Tarafa wa Tarafa ya Namanyere Wilayani Nkasi Kasim Ibrahim akitia saini
hati ya Makabidhiano mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa pamoja na Katibu
Tawala wa Mkoa ili kukabidhiwa Pikipiki aliyoahidiwa na Rais Dkt. John
Pombe Magufuli.
Kwa upande wake
Katibu Tawala huyo wakati akieleza mgawanyo wa pikipiki hizo alisema kuwa Mkoa
wa Rukwa una Tarafa 16 ambapo Tarafa 4 kati ya hizo zina pikipiki ambazo
zimekaguliwa na ziko salama zinaendeelea kufanya kazi na hivyo kuwasisitiza
maafisa hao kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika Waraka Namba 1 wa
Maendeleo ya Utumishi wa Umma wa Mwaka 2007.
“Tarafa ambazo hazikuwa
na usafiri kwa wilaya ya Kalambo ni Tarafa ya Matai, Kasanga, Mwimbi, Mwazye na
Mambwenkoswe zilikuwa hazina usafiri. Kwa Wilaya ya Sumbawanga ni Tarafa ya
Itwelele, Kipeta, Lwiche na Mtowisa na
Wilaya ya Nkasi ni Tarafa ya Chala, Kate na Namanyere na tarafa ambazo zilikuwa
na pikipiki kwa Wilaya ya nkasi ni Wampembe na Kirando na Wilaya ya Sumbawanga
ni Laela na Mpui,” Alisema.
Wakati akitoa neno la
shukrani kwa niaba ya Maafisa Tarafa wenzake, Afisa Tarafa ya Kasanga Andrew
Ngindo baada ya kumshukuru Rais Magufuli, alimuomba Mkuu wa Mkoa kuona
uwezekano wa kutengewa bajeti ya mafuta pamoja na matengezo kwa pikipiki hizo
ili ziendelee kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao.
“Kuwa na Pikipiki ni
jambo moja lakini pikipiki ikiwa bila ya Mafuta bila ya uwezeshwaji wa kutosha
ni kama tembo mweupe ndani ya nyumba, mimi niwaombe sana wakuu wa wilaya, sisi
ndio wawakilishi wao katika maeneo yale ambayo wao wasipofika sisi tukifika
maana yake Mkuu wa Wilaya amefika na tayari tumekuwa tumetekeleza makujumu yao,
kwahiyo Wakuu wa wilaya watusaidie kupata bajeti hiyo,” Alisema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli aliahidi kuwapa usafiri maafisa tarafa wote
nchini wasio na usafiri na hivyo kutoa pikipiki 448 kote nchini kwaajili ya
maafisa hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake.
No comments:
Post a Comment