NEWS

Friday, 13 February 2026

Butiama: Sagini apeleka kisima cha maji kwa wakazi 600 Makundusini




Na Mwandishi Wetu
Butiama
----------------

Wakazi zaidi ya 600 wa kitongoji cha Makundusini kilichopo katika kijiji cha Singu, kata ya Kukirango, wilaya ya Butiama mkoani Mara, wamenufaika na mradi wa maji uliofanikishwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Abdallah Sagini, kupitia Taasisi ya Direct Aid Society Tawi la Tanzania kutoka Kuwaït.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa kisima cha maji chenye uwezo za kuzalisha lita zaidi ya 20,000 kwa siku, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, alipongeza juhudi zilizofanywa na Mbunge Mstaafu wa Jimbo hilo, Sagini, kwa kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sera ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

Katika hotuba yake, DC Thecla alisema mradi huo utasaidia wananchi wa eneo hilo kuondokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Direct Aid Society Tawi la Tanzania kutoka Kuwaït, Abdelhamid Ismail, alisema taasisi hiyo ilianza kutoa huduma nchini Tanzania tangu mwaka 1987 na tayari ipo katika kanda tano ambazo ni Tanga, Moshi, Kigoma, Singida na Dar es Salaam.

Abdelhamid alisema kupatikana kwa mradi huo wa kisima cha maji katika kitongoji cha Makundusini ni sehemu ya matunda ya urafiki na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya taasisi hiyo na Sagini, ambapo aliiunganisha na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassim, alisema kuwepo kwa mradi huo ni mawazo ya Sagini tangu aliponunua eneo hilo na kulikabidhi, ambapo walishirikiana na BAKWATA na akawa na mikakati ya kupeleka miradi mingi maeneo mbalimbali ya wilaya ya Butiama, ukiwemo huo wa kisima cha maji.

Diwani wa Kata ya Kukirango, Rajab Mjengwa, alieleza kuwa ni jukumu lao kuhakikisha huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa wakazi wote wa kitongoji cha Makundusini na vitongoji jirani.
Diwani wa Viti Maalum Wilaya ya Butiama, Amina Ally Solis, alishukuru kuwepo kwa mradi huo akisema umepunguza adha kwa kina mama na watoto waliokuwa wanalazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya sita kutafuta maji.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Singu, Bitarus Mkono, aliwashukuru wafadhili hao - Taasisi ya Direct Aid Society Tawi la Tanzania kutoka Kuwaït na Mbunge aliyepita, Sagini, kwa kusilikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, ikiwemo ya maji kijijini hapo.

Wanawake wakipata huduma ya maji safi na salama katika mradi wa kisima hicho

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages