NEWS

Wednesday 22 April 2020

Kuingia hospitali Bariadi sasa lazima kuvaa barakoa


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga akihimiza wananchi kujikinga na ugonjwa wa COVID-19


Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Dkt Judith Ringia, amesema wananchi wote watakaohitaji huduma katika hospitali ya halmashuari hiyo (Somanda) watatakiwa kuvaa barakoa kama moja ya hatua za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) kuanzia wiki ijayo.

Aidha, Dkt Ringia amesema kila mwananchi atapimwa joto la mwili kabla ya kuingia na kutoka hospitalini na kwamba watoa huduma wote watakuwa vifaa kinga.

Dkt Ringia amesema hayo jana Aprili 21, 2020 mara baada ya uzinduzi wa kutembelea na kutoa elimu katika maeneo ya mikusanyiko juu ya kujikinga na virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
DC Kiswaga  na viongozi wengine wakitoa elimu  ya kujikinga na Covid 19 kwa wananchi 
“Tumeweka mazingira salama kwa watumishi wetu, ambapo kwa sasa kila mtumishi anavaa barakoa na wao tunawapima joto la mwili kabla ya kuingia na kutoka ndani ya hospitali, pamoja na hayo, tutatembelea maeneo yote ya minada, magulio, masoko na stendi za mabasi na tayari kikosi maalumu kimeundwa kwa ajili ya kutoa elimu hiyo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Festo Kiswaga, ambaye ni mwenyekiti wa timu hiyo, amewataka wananchi wanaokwenda kutafuta mahitaji kwenye minada, magulio na sokoni kuhakikisha wanachukua tahadhari ikiwemo kunawa mikono.

Sambamba na hilo, Kiswaga amewataka wafanyabishara kuhakikisha wanaweka ndoo ya maji tiririka na sabuni katika maeneo ya biashara zao na kwamba wananchi wanatakiwa kununua bidhaa na kuondoka mara moja.

(Habari na Anita Balingilaki, Bariadi)


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages