KITUO
cha kulea watoto cha Bikra Maria kilichopo Lamadi wilayani Busega, Simiyu
chenye watoto wenye umri wa kuanzia miezi miwili hadi miaka 18, kimepokea
msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19) na
vyakula kutoka JBS Fuel Co. Ltd.
Msaada
huo uliokabidhiwa leo Aprili 22, 2020 unahusisha vitakasa mikono, sabuni za
maji, ndoo kwa ajili ya kunawia mikono, mahindi na sukari, vyote vyenye thamani
ya Sh milioni mbili.
Awali,
akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Lucy Sabu, amesema ameguswa
kutoa vifaa na vyakula hivyo kuwasaidia watoto hao kipindi hiki cha tahadhari
dhidi ya COVID-19.
“Kwa
dhati ya moyo wangu nimeamua kuungana na serikali kuhakikisha hakuna maambukizi
zaidi ya ugonjwa wa corona, lakini pia mahindi na sukari vitasaidia kwa
chakula,” amesema Sabu.
Mkurugenzi
huyo amewataka wadau wengine wakiwemo watu binafsi kujitokeza kwa wingi kusaidia
makundi yenye mahitaji maalumu katika jamii wakiwemo watoto.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera, amemshukuru mkurugenzi huyo
na kuwaomba wadau wengine kuunga mkono jitihada za serikali katika kudhibiti
janga hilo la kimataifa.
Naye
Mratibu wa magonjwa yanayosababishwa na virusi vya Corona na Ukimwi Mkoa wa
Simiyu, Dkt Khamis Kulemba, ameutaka uongozi wa kituo hicho kuongeza
maeneo ya kunawia mikono na kuwasisitiza watoto kunawa mara kwa mara.
Mkurugenzi
wa kituo hicho, Sista Helena Ntabulwa, amesema kinalea watoto 71
kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwemo waliofiwa wazazi, waliotelekezwa
na wenye ulemavu wa ngozi.
Sista
Ntabulwa ameipongeza serikali mkoani Simiyu chini ya Mkuu wa Mkoa, Anthony
Mtaka, akisema imekuwa bega kwa bega na kituo hicho kwa kusaidiana na wadau
mbalimbali wenye mapenzi mema na watoto.
Katika
hatua nyingine, mjumbe wa bodi ya kituo hicho, Belensi China, amesema kinakabiliwa
na changamoto ya fedha za kugharimia matibabu ya watoto, mishahara ya
wafanyakazi na chakula, hivyo kuomba wadau kuendelea kuwasaidia.
(Habari na Anita
Balingilaki, Busega)
No comments:
Post a Comment