NEWS

Sunday 12 April 2020

Mtaka: Watoto waepushwe kwenye mikusanyiko


Mkuu wa Mkoa wa Simuyu, Anthony Mtaka
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka wazazi na walezi kutoambatana na watoto wadogo katika maeneo ya mikusanyiko ya watu kama vile ibadani, masoko na minada ili kuwaepusha dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ukiwemo COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Badala yake, Mtaka amewataka kuwaacha watoto nyumbani katika mazingira yaliyo na tahadhari dhidi ya ugonjwa huo hatari, kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali.

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amesema ni vizuri watu wenye umri mkubwa na wale wenye magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kisukari na shinikizo la damu kuepuka kuhudhuria maeneo hatarishi kiafya.

Mtaka ameyasema hayo kwa nyakati tofauti leo Aprili 12, 2020 alipotembelea makanisa mbalimbali mkoani Simiyu wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.

“Mzazi/mlezi unapokuja kanisani watoto wako waache nyumbani, ukifika waombee wakiwa huko (nyumbani) na kama tuna wazazi wetu ambao umri umeenda nao ni vema wakabaki nyumbani,” amesema Mtaka na kuongeza:

“Kila mara mnasika kauli ya Rais wetu mpendwa Dkt Magufuli, mnasikia kauli ya Waziri wa Afya kupitia vyombo mbalimbali vya habari, fateni maelekezo hayo, chukueni tahadhari.”

Hata hivyo, amewataka wananchi wote kuendelea na utaratibu wa kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia vitakatisha na maji tiririka hata wawapo nyumbani kujikinga na janga la COVID-19.

Kuhusu wanafunzi walio nyumbani baada ya shule kufungwa ili kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19, Mtaka amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanajisomea.

“Mitiani ya kitaifa ipo pale pale, wazazi na walezi wahimizeni watoto wenu kujisomea hata kama wanawasaidia kazi mbalimbali za nyumbani watengeeni muda wa kujisomea, kikubwa hapa kabla ya kuanza masomo wahakikishe taratibu zote za kiafya zinafuatwa ili kujikinga na ugonjwa huu.

“Hii likizo si ya watoto kuzurura ovyo, tusijefungua shule zetu watoto wakiwa na mimba, kaeni chini na watoto wenu mzungumze nao, amesisitiza Mtaka.

Katika hatua nyingine, Mtaka amewataka wananchi mkoani Simiyu kuweka akiba ya chakula kutokana na msimu huu kupata ziada na si kuuza chote baadaye wajikute wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Kwa upande wao, viongozi wa dini akiwemo Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Luka, Padre Martine Jilala, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) la mjini Bariadi, Greyson Kinyaha, Mchungaji wa African Inland Church of Tanzania (AICT) Bariadi, Amosi Ndaki na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu John, Padre Peter Mkunya, wametumia maadhimisho ya Ufufuko wa Yesu Kiristo (Pasaka) kumwomba Mungu kuliepushia taifa janga la COVID-19.

Koga Mihama na George Lyimo ambao ni miongoni mwa waumini waliohudhuria ibada ya Pasaka wameishukuru serikali kwa kuendelea kuchukua hatua na kuhimiza wanachi kujikinga dhidi ya janga hilo la dunia.

( Habari na Anitha Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages