NEWS

Sunday 17 May 2020

Ajenda ya Nikodemus Keraryo 2020


*Atamani Tarime Vijijini yenye uchumi wenye tija

KATIKA kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini, wanasiasa wengi wameona umuhimu wa kuweka wazi ajenda na matamanio yao juu ya maendeleo ya wananchi.

Miongoni mwao ni kijana msomi na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nikodemus Kerarya maarufu zaidi kwa jina la Nico, mkazi wa jimbo la Tarime Vijijini.
Nico akizungumza katika hafla ya kuchangia vikundi vya maendeleo 

Katika mahojiano maalumu na  gazeti la Sauti ya Mara  hivi karibuni, Nico ameweka bayana ajenda yake kuu kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kuwa ni kuona Tarime Vijijini ikistawi kwa uchumi wenye tija kwa wakazi wake.


Yafuatayo ndio mahojiano yenyewe:

Sauti ya Mara: Ndugu Nico, wewe ni kijana ambaye umekuwa na mitazamo chanya katika masuala ya maendeleo ya wananchi. Una ajenda gani ya msisimko wa kimaendeleo kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini?

Nico: Ajenda yangu kuu na muhimu kipindi hiki ni Tarime Vijijini yenye uchumi wenye tija wananchi.

Tarime ni wilaya iliyojaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za uchumi. Hata hivyo, tunapaswa kuzitambua fursa za uchumi kwa tija ya maendeleo yetu.
Nico akikagua miradi ambayo inaweza kuwakomboa vijana

Tarime Vijijini tunahitaji viwanda, hii ni kwa sababu zipo fursa za kilimo, mazao yote yanakubalika huku.

Pia zipo fursa za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu. Maeneo mengi Tarime Vijijini yamezungukwa na madini.

Hivyo, kama utaratibu wa msingi utafanyika wa kuwatafutia wachimbaji wadogo wadogo maeneo mbadala ya uchimbaji, kipato cha wananchi kitaongezeka maradufu.

Sauti ya Mara: Ni mambo gani hasa ambayo unaona bado yanahitaji msukumo zaidi kutoka kwa viongozi watakaopatikana kupitia uchaguzi mkuu ujao?

Nico: Yapo mambo mengi ya kiutendaji na uwajibikaji kwa viongozi.

Kwanza, jamii ya Tarime Vijijini inahitaji maji safi na salama kwa matumizi mbalimbali.

Maeneo mengi ya jimbo hili yana changamoto kubwa ya maji. Hivyo, kiongozi/viongozi watakao pata fursa ya kuwakilisha wananchi lazima washughulikie changamoto ya maji.

Pili, jimbo letu lina changamoto kubwa ya barabara. Mfano, barabara itokayo Tarime, Nyamwaga, Nyamongo hadi wilaya ya Serengeti ni muhimu kama kiunganishi cha wilaya hizi, lakini pia ni njia kuu ya watalii watokao nchini Kenya kuelekea hifadhi za Serengeti na Ngorongoro.

Zipo pia barabara nyingi zenye changamoto kubwa lakini ni muhimu kwa uchumi wetu, hasa katika usafirishaji mazao na mifugo. Watakaopata fursa walishughulikie hilo.

Tatu, kuna baadhi ya maeneo yanapaswa kupewa hadhi ya mamlaka ya mji; kama vile mji wa Nyamongo na Sirari. Suala hili limezembewa, hivyo kuendelea kufifiisha jitihada za maendeleo katika sehemu hizo.

Nne, yapo masuala ya huduma za afya. Hili bado ni tatizo, hasa mfumo utumikao sasa wa kupata dawa katika vituo vyetu vya afya na masuala mengine ya uendeshaji. Changamoto ya afya ni kubwa kulingana na matarajio ya wengi.

Tano, ili kuweka kiunganishi cha wakulima na wafanyabiashara, eneo la Sirari linapaswa kuboreshwa na kuweka soko la kimataifa la mazao.

Kwa kuwa eneo hilo ni mahususi kama njia kiunganishi ya mikoa mbalimbali, ni vyema ikawa Center of Collections (kituo cha ukusanyaji) ya mazao ya kilimo na kukuza uchumi.

Sauti ya Mara: Wewe binafsi umejipangaje na ushiriki wako wa moja kwa moja katika hayo utakuwaje?

Nico: Suala kubwa na la msingi kwanza, nimejiandaa kwa kuhakiki taarifa zangu za mpigakura.

Lakini pia nimejiandaa kushiriki katika uchaguzi, hasa katika nafasi ya kuchagua na kuchaguliwa. Na kwa kuwa ni haki yangu kikatiba, nitayatimiza yote kwa utashi wangu na kwa mujibu wa sheria za nchi.
Nico akiwa katika shughuli za ujenzi wa chama(CCM)

Sauti ya Mara: Kwa muda mrefu sasa umekuwa msaada kwa vijana wa jinsia zote, hasa katika masuala ya ujasiriamali na uwezeshwaji. Je, unadhani bado kundi hilo la jamii linahitaji kupewa kipaumbele katika masuala ya kujikwamua kiuchumi?

Nico: Ndiyo. Kwanza, ifahamike kuwa vijana ni kundi muhimu linaloweza kuzalisha kwa ziada nchini. Pia vijana ni kundi lenye wajibu wa kuilinda jamii katika masuala yote ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Hivyo, kuna haja ya kuendelea kulisaidia kundi hili kwa kuliwezesha kiuchumi. Mfano, kupewa mikopo yenye riba nafuu au isiyokuwa na riba kabisa, kuliwezesha katika fikra za uzalishaji mali na uongozi thabiti wa kimkakati na kimaendeleo.
Nico akiwa akihamasisha maendeleo 

Tuna wajibu wa kuwafanya vijana kuwa sehemu timilifu ya jamii yetu katika nyanja zote za uwajibikaji.

Sauti ya Mara: Ungependa kuona vijana wanawezeshwa zaidi katika nyanja gani?

Nico: Kwanza, mikopo yenye riba nafuu au isiyo na riba. Pili, wapewe na waaminiwe katika fursa za uongozi na hasa nafasi za uwakilishi wa jamii katika taasisi mbalimbali. Tatu, washirikishwe katika maamzi mbalimbali yahusuyo maisha ya jamii yao.

Sauti ya Mara: Tumeona umekuwa muumuni mzuri wa kuhamasisha vijana kufikiria kuisaidia nchi badala ya kutaka nchi ndiyo iwasaidie. Je, ni mambo gani makubwa na yenye maslahi mapana ya umma ambayo wewe kama kijana umeweza kuisaidia nchi kupitia kwa wananchi?

Nico: Ni kweli nimeshiriki katika hamasa mbalimbali za kimaendeleo katika jamii yangu na hata kujitolea kwa rasilimali fedha, nguvu na ushawishi ili jamii yangu isonge mbele. Yapo mambo kadhaa nimeweza kuyafanya.

Nico(kulia) akikabidhi msaada wa  mifuko ya Saruji

Moja, nimeshiriki katika masuala ya uundwaji wa vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na kuvisimamia ili vifikie mafanikio. Mfano, ni Jikomboe, Mbuya Honey, Mt. Anna, Nyada, Nyabibago, kwa kutaja baadhi.

Pia nimekuwa mwakilishi wa jamii ya Nyamongo katika Mfuko wa Dhamana wa Jamii ya Mara Kaskazini, nimefanikiwa kuishawishi taasisi hii kupima viwanja (kurasimisha makazi) zaidi ya 12,000 katika miji ya Nyamongo na Nyamwaga.

Aidha, nikiwa nafanya kazi katika mgodi wa North Mara, nilifanikiwa kuushawishi uongozi wa mgodi huo kufanya marekebisho ya miradi mbalimbali ya jamii kupitia mikataba halisi na jamii, yaani Village Benefit Agreement - VBA na Village Benefit Implementation Agreement - VBIA.

Pia nimefanikiwa kuushawishi uongozi wa mgodi huo kuanzisha tamasha la wajasiriamali linalosaidia jamii iliyo jirani kuzitambua fursa za maendeleo na uchumi.
Nico(wakwanza kulia) akiwa katika hafla ya kuendeleza sekta ya michezo

Vilevile, nilifanikiwa kushawishi uanzishaji wa tamasha la michezo linalosaidia kuibua vipaji mbalimbali vya vijana na kuwajenga kiafya, kiakili na kujipatia ajira. Hayo nimetaja baadhi tu miongoni mwa mengi niliyowezesha.

Sauti ya Mara: Je, unaridhika na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, hususan katika jimbo la Tarime Vijijini ambako wewe ni mzaliwa na mkazi wa huko?

Nico: Kwa maana ya uwajibikaji wa chama changu cha CCM, viongozi wamejitahidi kusaidia hatua mbalimbali za kutatua migogoro mikubwa ya jamii katika nyanja tofauti.

Serikali kupitia halmshauri imesaidia katika ujenzi wa miundombinu kulingana na bajeti, japo jitihada kubwa zinahitajika ili kuiona Tarime Vijijini imebadilika kiuchumi na kimaendeleo.
Nico anaamini kilimo cha bustani bora kinaweza kukomboa vijana

Sauti ya Mara: Mwisho unadhani wapigakura wazingatie vigezo gani kuhakikisha wanatumia haki zao za kidemokrasia na kikatiba katika kuwapata viongozi watakaowatumikia kwa kiwango cha kuridhisha?

Nico: Kwanza, mwakilishi wa wananchi awe ni mtu anaezitambua vyema changamoto za wananchi wa jimbo la Tarime Vijijini, sio za kuambiwa tu, bali azijue na aziishi katika hatua mbadala, yaani kwa kuzitafutia ufumbuzi.
Nico akihamasisha  ufugaji kuku

Pili, awe mkazi wa jimbo hili, sio mbeba begi anayetaka uongozi wa tumbo lake na familia yake binafsi badala ya wananchi kwa jumla.

Tatu, awe na uwezo mbadala wa kuzitambua fursa za maendeleo na si tu kutegemea Serikali Kuu.

Nne, awe na uwezo wa kufanya siasa za maendeleo na si siasa za siasa.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages