NEWS

Sunday 3 May 2020

HAMIS MKARUKA: Wanaume tusiwakwaze wanawake wanaojitokeza kugombea uongozi

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime Hamis Mkaruka

Baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwanyima wanawake uhuru wa kugombea nafasi za uongozi kutokana na dhana potofu kwamba mwanamke akipata madaraka atamtawala mwanaume au kushindwa kuihudumia familia.

Huo ni mfumo dume na imani potofu. Wanaume wanatakiwa kubadilika na kuwaunga mkono wanawake wanapojitokeza kugombea uongozi ili kutimiza adhima ya kuwa kiongozi katika jamii na taifa.

Hamis Mkaruka ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara. Anasema kikwazo kikubwa cha mwanamke kugombea ni baadhi ya wanaume, hasa walioko kwenye ndoa hawawapi wake zao nafasi ya kufanya kampeni jambo linalosababisha baadhi yao kukosa nafasi za uongozi.

“Shida iko kwa wanaume, wamekuwa kikwazo kwenye familia, kuna mwanamke kata ya Mwema alijitokeza kugombea uenyekiti wa kitongoji, kachukua fomu kajaza lakini mume alimzuia kugombea akisema akiwa mwenyekiti atamtawala, mawazo ambayo ni imani tu za watu,” anasema Mkaruka.

Anaongeza “Mwanamke kuongoza siyo kwamba ndiyo atatawala hadi nyumbani na tuelewe siyo kweli kwamba mtu kuwa kiongozi anabadilika, kama ana tabia ya kukutawala atakutawala tu hata kama si kiongozi. Watu wabadilike na wawape fursa wanawake wagombee uongozi.”

Mkaruka anasema wanawake wakiwa kwenye madaraka wanasaidia kutoa hoja na wasipokuwepo ni athari kwa kuwa pale zitakapotokea hoja zinazohusu mwanamke zinakuwa hazina utetezi yakiwemo masuala ya afya ya mama na mtoto na ukatili wa kijinsia.

 Anasema katika uteuzi wa wagombea, CCM kimekuwa kikiwajali wanawake kwa kuwateua kuwania nafasi za uongozi, lakini kumekuwa na shida ya kutochaguliwa na wanachama kwenye kura za maoni na za jumla katika Uchaguzi Mkuu na wa Serikali za Mitaa.

“Chama chetu wanapojitokeza wagombea, nafasi tatu lazima awemo mwanamke, ndio utaratibu wa chama, shida inakuja pale chama kimempitisha lakini jina likienda kwa wapigakura hachaguliwi au akichaguliwa kwenye chama akienda kugombea wananchi hawampigii kura,” anasema Mkaruka.

Katibu huyo wa CCM anasema wilaya ya Tarime ina kata 34, vijiji 88, mitaa 81 na vitongoji 500, ikiwa na majimbo mawili ambayo ni Tarime Vijijini na Tarime Mjini na kwamba kuna idadi ndogo ya wanawake viongozi ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanaume wanaongoza.

Anasema licha ya wilaya kuwa na kata 34, katika nafasi ya uenyekiti wa CCM kata, yupo mwanamke Hidaya Philipo aliyeshinda katika kata ya Gwitiryo na wengine wawili walishinda nafasi ya uenezi ngazi ya kata na jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Tarime.

Katika nafasi ya ubunge kwenye majimbo yote mawili, Mkaruka anasema CCM hakina mbunge; waliopo ni wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema), mmoja akiwa ni mwanamke Esther Matiko wa Tarime Mjini.

Anasema CCM pia hakina diwani mwanamke wa kuchaguliwa katika kura za jumla isipokuwa kina madiwani wanne wa viti maalumu, ambapo kwa upande wa Chadema kuna madiwani wawili wa kuchaguliwa.

Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, CCM kinaongoza ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji kwani wengi wao walipita bila kupingwa baada ya vyama vya upinzani kujiondoa kwenye uchaguzi huo.

Mkaruka anafafanua kwamba katika wilaya hiyo, wanawake waliogombea kwenye kura za maoni ndani ya CCM walikuwa wanne na wote hawakushinda. Katika mitaa 85 wanawake watano waligombea, kati yao, watatu walishinda.

Anasema kuna vitongoji 500, kati ya hivyo, wanawake 55 walijitokeza kugombea na walioshinda ni 32, nafasi zilizobaki walishinda wanaume.

Mkaruka anasema elimu zaidi ya kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea inahitajika, lakini pia wananchi wawaamini na kuwachague.

Anasema kumekuwepo mfumo dume kwamba mtu akiteuliwa viti maalumu anaonekana hana uhalali licha ya kwamba nafasi hizo zinaongeza idadi ya wanawake.

Kusipokuwa na viti maalumu wanaume watakuwa wengi na utetezi wa masuala ya wanawake hautakuwepo,” anasema Mkaruka.

Anawataka wanawake ambao wamekuwa viongozi kwa nafasi za viti maalumu kuwaachia wengine nafasi hizo na kwenda kugombea nafasi za kuchaguliwa, badala ya kuendelea kung’ang’ania viti hivyo.

Mkaruka anasema kumekuwa na tabia ya baadhi ya madiwani na wabunge wa kuteuliwa kutoshirikiana katika maendeleo huku wa viti maalumu wakishindwa kufanya kazi kwa kisingizio kuwa ni wa viti maalumu au akifanya mkutano wale wa kuchaguliwa huwaona wanataka kuwachukulia nafasi zao.

“Mbunge au diwani wa viti maalumu wao wanajikita na masuala ya wanawake, lakini mbunge wa jimbo au diwani wa kata yeye anashughulika na watu wote wakiungana na kufanya kazi kwa pamoja kuchochea kasi ya maendeleo. Diwani au mbunge wa viti maalumu anaruhusiwa kufanya mkutano, kwa hiyo wasijidharau,” anasema Mkaruka. 
Akizungumzia suala la wanawake wengi kujikita katika kugombea viti maalumu, Katibu wa UWT Wilaya ya Tarime, Sauda Kashombo, anasema sasa ni wakati wa wanawake kujipima kugombea nafasi za uchaguzi kwani hatua hiyo huwajenga zaidi na kukubalika kwani wanakuwa wamechaguliwa na wananchi.

Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake ya 2019/2020 iliyoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Mtandao wa Wanawake na Katiba, Uchaguzi na Uongozi, inaonesha kuwa uchaguzi wa mwaka 2015 ulivunja rekodi ya kumchagua Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke tangu nchi ipate uhuru, katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli.

Ilani hiyo inaonesha tamwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) za Uchaguzi Mkuu za mwaka 2015 katika ngazi ya uwaziri ni asilimia 17, makatibu wakuu asilimia 11 na wakuu wa mikoa asilimia 23 ikilinganishwa na asilimia 28.5 kipindi cha 2010/2015 ambapo wakuu wa wilaya walikuwa asilimia 28 kutoka asilimia 35.3 ya nyuma.

Ilani hiyo inaeleza kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uchaguzi bado ni mdogo ambapo idadi ya wanawake wanaoteuliwa na vyama vya siasa kuwania nafasi za ubunge wa kuwakilisha jimbo ni ndogo, wanaoshinda ni ndogo zaidi na wachache huteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi za uchaguzi.

Uchaguzi wa mwaka 2015 wanawake walioteuliwa na CCM kugombea uongozi ni asilimia tisa, Chadema asilimia sita, CUF asilimia 11 na ACT Wazalendo asilimia 15.

Kulikuwa na wagombea wa viti vya ubunge 1,250 kwa Tanzania Bara, kati yao, wanawake walikuwa 238 sawa na asilimia 19.

Katika ngazi ya udiwani, kati ya wagombea 10,879, wanawake walikuwa 679 sawa na asilimia 6.2.

Hivyo hatua za makusudi zisipochukuliwa kurekebisha hali hiyo, itachukua chaguzi 31 au miaka 155 kurekebisha pengo hilo la jinsia.

Inaelezwa kuwa viti maalumu vimewezesha ongezeko la wanawake katika vyombo vya uwakilishi.

Akitolea mfano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la tisa lilikuwa na wawakilishi wanawake kupitia viti maalumu 75 sawa na asilimia 74.2 ya wabunge wanawake.

Mtandao huo wa kijinsia unabainisha kuwa idadi hiyo iliongezeka kufikia 102 sawa na asilimia 78.5 ya wabunge wote wanawake. Katika Bunge la 11 idadi iliongezeka hadi 113 sawa na asilimia 79.3 kati ya wabunge wanawake 145.

Ilani hiyo ya uchaguzi wa wanawake inaeleza kuwa bado kuna changamoto ya wawakilishi wanaopitia viti maalumu ambao hubaguliwa katika kushika baadhi ya nyadhifa kama vile ya uwaziri mkuu, hubaguliwa katika kupewa fedha za majimbo na kwenye baadhi ya vyama vya siasa hakuna uwazi kwenye uteuzi.

(Makala na Dinna Maningo, Tarime)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages