MTOTO wa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere, Madaraka Nyerere, ametangaza kuwania nafasi ya ubunge
katika jimbo la Butiama mkoani Mara, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Sijatumwa na mtu yeyote
kuomba nafasi hii ila nimejipima uzoefu na uwezo wangu na kuamua kuwa ni wakati
muafaka sasa wa kutumia uwezo na uzoefu huo kutumikia jamii pana zaidi,” mtoto
huyo wa Baba wa Taifa amewaambia waandishi wa habari.
“Ni kwa sababu sijatumwa
na mtu ndio maana leo hii mnaniona niko hapa peke yangu kutoa tamko hili, kwa
sababu pamoja na kwamba nahitaji uungwaji mkono wa Chama Cha Mapinduzi na
wapigakura wa Butiama, hatua ya kwanza ninataka kuifanya mwenyewe kwa kuamini
kwamba ninaweza kupokea majukumu nitakayokabidhiwa.”
Amesema jambo la kwanza
lililomsukuma kuwania nafasi hiyo ni baada ya kuona Mwenyekiti wa CCM Taifa,
Rais Magufuli amejenga mazingira mazuri yanayomwezesha mwanachama yeyote wa
chama hicho kugombea uongozi na kupata haki bila kujali uwezo wake wa kifedha
wala ukaribu wake na viongozi wa juu.
“Pili, Mheshimiwa Magufuli
ni kiongozi ambaye tumeona ameweka jitihada kubwa sana za kutanguliza maslahi
ya Taifa mbele, kwa hiyo katika mazingira kama hayo na mimi nikijipima na imani
zangu nafikiri itakuwa ni heshima kubwa sana ya kufanya kazi pamoja na kiongozi
kama huyo kwa sababu naamini yale anayoamini yeye… naweza kuwa askari mzuri wa
kufanya naye kazi,” ameongeza Madaraka.
Mbunge wa jimbo la Butiama
aliyemaliza muda wake ni Nimrodi Mkono (CCM).
(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Butiama)
No comments:
Post a Comment