NEWS

Saturday 6 June 2020

Majaribio chanjo ya mRNA1273 mwanga mpya dhidi ya corona
























CHANJO ni kitu pekee kinachoweza kupunguza maambukizi na kuondoa kabisa ugonjwa wa corona ambao mpaka sasa umewapata watu zaidi ya milioni tano na kusababisha vifo zaidi ya laki tatu duniani.

Kwa kulitambua hili, kampuni nyingi za dawa na vyuo vingi vilianza mchakato wa kupata chanjo ikiwemo Pfizer na mshirika wake BioNTech, kampuni kutoka China, Cansino na Chuo Kikuu cha Oxford kinachoshirikiana na AstraZeneca.

Leo nitaongelea chanjo iliyofikia hatua ya majaribio kwa binadamu inayoonesha matumaini makubwa.

Chanjo hii inajulikana kitaalamu kama mRNA1273 kutoka kwenye kampuni ya Moderna kwa kushirikiana na kitengo cha taifa cha mzio (Allergy) na magonjwa ya kuambukizwa cha Marekani chini ya uongozi wa Profesa Fauchi.

Profesa Fauch ni mwanasayansi mkongwe ambaye ameishauri Serikali ya Marekali kipindi hiki cha mlipuko wa corona, lakini pia aliishauri Serikali ya Rais Barack Obama na Gorge W. Bush wakati wa magonjwa mengine ya mlipuko.

Ijue mRNA1273

Hii ni chanjo ya kwanza kujaribiwa kwa binadamu iliyofanya mwili kutengeneza kinga dhidi ya virusi vya SAR-CoV 2 vinavyosababisha ugonjwa wa corona, hivvo kutoa mwanga mkubwa kwa dunia inayohaha kupata suluhisho la ugonjwa huu wa mlipuko.

Muundo wa chanjo hii

Wamechukua sehemu ya vinasaba vya SARS-CoV-2 viitavyo kitaalamu messenger RNA. Kwenye hatua ya kwanza ya majaribio walichoma watu wanane wenye umri wa miaka 18 hadi 55 wenye afya njema ambao hawajawahi kupata maambukizi ya corona.

Dozi zilikuwa za aina tatu, ndogo, ya kati na kubwa. Madhara mbalimbali yalipatikana kutona na dozi zilizotolewa kwa wajaribiwa.

Madhara ya dozi ndogo na ya kati yalikuwa wekundu na maumivu kwenye eneo ambalo mtu alichomwa chanjo, wakati madhara yaliyotokana na kuchomwa dozi kubwa yalikuwa homa kali na maumivu ya misuli.

Kiasi cha kinga kilionekana kuwa sawa bila ya kujali kiasi cha dozi, hivyo kufanya dozi ndogo tu ya kiasi cha 25 µg kuwa changuo wakati majaribio yakiendelea. Waliojitolea kuwa sehemu ya majaribio ya chanjo hii walichomwa dozi mbili, dozi ya pili unaipata juma la nne baada ya dozi ya kwanza.

Walipochukua kinga zilizotengenezwa na mwili dhidi ya SARS-CoV 2 na kuzichoma kwenye seli ya mwili iliyoathirika na virusi vya corona. Kinga hii iliweza kuvifubaza kabisa virusi hivyo.

Japokuwa idadi ya watu ni ndogo, matokeo haya yanaonyesha mwanga mkubwa mbele. Majaribio ya chanjo ya mRNA1273 kwenye hatua ya kwanza yanaendelea na makundi mengine mawili yataongezwa, yaani kwa watu wenye umri wa miaka 55 hadi 70 na wenye miaka 71 na zaidi.

Mpaka sasa Moderna hawajasema chochote kuhusu kuwaweka watoto kama sehemu ya majaribio na sababu ya msingi ni kwamba majaribio kwa watoto huwa yanachelewa mpaka chanjo inapoonesha ni salama kwa watu wa wenye umri mdogo (young adults).

Hatua ya pili ya majaribio inatarijiwa kuanza mapema na itahusisha takribani watu 600 na hatua ya tatu inatarajiwa kuanza Julai mwaka huu.

Iwapo chanjo hii itafanikiwa, itapatikana kwenye mzunguko mwisho wa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka 2021.

Tanzania, nchi zinazoendelea zitapataje chanjo hii?

Kuna mashirika mengi ya misaada duniani yakiwemo Gavi na Vaccine Alliance ambayo yamesaidia sana nchi maskini kupata chanjo za magonjwa mengine mengi ya kuambukiza. Mashirika hayo yako mstari wa mbele kuhakikisha ulimwengu unapata kwanza chanjo salama na bila shaka yatashiriki kikamlifu kuhakikisha watu walio na uchumi mdogo wanapata chanjo.

Mfano kwa miongo miwili iliyopita, Gavi kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Watoto (UNICEF), yamefanikisha huduma za chanjo kwa nchi 73 maskini duniani.

Gharama za utafiti wa chanjo hii ni kubwa na ukiongeza tena na gharma za upatikanaji wa chanjo ya corona, gharama zinaweza kuwa kubwa Zaidi, lakini hakuna gharama kubwa kama kuacha ugonjwa huu uendelee kuwepo.

Kitu cha msingi ni kwamba nchi zilizoendelea zitambue kwamba chanjo ni huduma ya msingi kwa kila mtu, hivvo chanjo haina budi kuwa na bei nafuu.

Dunia itakuwa salama pale kila nchi itakapokuwa salama bila kuangalia hatua ya maendeleo iliyofikia.


(Na Daktari Shally Zumba Mwashemele
Simu: +255 716 615 651

Barua Pepe: shallyzumba@gmail.com)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages