NEWS

Wednesday 24 June 2020

Milioni 249 zaboresha huduma zahanati ya Old Maswa

Shilingi milioni 249.4 zimetumika kugharimia uchimbaji wa kisima cha maji, ujenzi wa jengo la Huduma ya Tiba na Matunzo (CTC) na ukarabati wa zahanati ya Old Maswa inayomilikiwa na Kanisa Katoliki wilayani Bariadi, Simiyu.

Kati kiasi hicho cha fedha, shilingi milioni 39.53 zimegharimia uchimbaji wa kisima, ukarabati wa matenki na mabomba ya kuvuna maji ya mvua, na shilingi milioni 209.88 zimetumika kugharimia ujenzi wa na ukarabati wa majengo ya zahanati hiyo.
Makamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Padre Kizito Nyanga akiongea kabla ya uzinduzi wa jengo jipya la CTC.

Fedha hizo ni ufadhili kutoka shirika lisilo la kiserikali la Doctors with Africa (Cuamm) linalofanya kazi na mkoa wa Simiyu kama mdau wa afya katika masuala ya Ukimwi na huduma za afya ya mama na mtoto.

Hayo ni kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Old Maswa, Dkt Ndaro Lawi, wakati akisoma risala ya uzinduzi wa jengo jipya la CTC juzi, ambapo tayari wameandikisha wahitaji 219 wa huduma hiyo.

Paroko wa Parokia ya Old Maswa, Padre Paul Kitali, amesema kisima hicho kina uwezo wa kutoa lita 2,500 za maji kwa saa na kwamba wananchi wamekuwa wakichangia shilingi 500 kwa madumu sita yenye ujazo wa lita 20 kwa kila moja.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Festo Dugange, Mratibu wa Kuthibiti Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wa Mkoa huo, Dkt Khamis Kulemba, amesema kituo hicho kitasaidia jamii na kutumia nafasi hiyo kutoa wito kwa walioanza kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo kutozipuuza kwa kigezo cha kuombewa na kuamini wamepona.


"Baadhi ya madhehebu yanaleta vikwazo katika matibabu ya Ukimwi, unakuta baadhi wanasema maombi yanaponya, watu wanaacha dawa na kutengeneza usugu wadudu na mgonjwa anazidiwa," amesema Kulemba.

Kwa upande wake, Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Padre Kizito Nyanga aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amesema kanisa hilo lina kiu ya kuwafikia watu kwa matendo (huduma) na lipo tayari kushirikiana na wote wanaotoa huduma, ndio maana likafungua mlango kwa Cuamm kwa lengo la kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Magufuli.

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages