NEWS

Friday 7 August 2020

KASODEFO yang’ara ushauri wa kisheria Nanenane Simiyu

 

Msaidizi wa Kisheria, Sarah Maduka (kushoto), akitoa elimu ya namna ya kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya ukatili kwa baadhi ya wananchi wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi waliofika kwenye banda la KASODEFO katika maonesho ya Nanenane, Nyakabindi.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Kawiye Social Development Foundation (KASODEFO) lenye makao makuu wilayani Maswa kwa kushirikiana na shirika la Legal Services Foundation (LSF) limewafikia wananchi 1,900 wakiwamo 56 wanaohitaji msaada wa kisheria juu ya migogoro ya ardhi, ndoa, ukatili wa kijinsia na mirathi, waliotembelea banda lao kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi, Simiyu.

 

Aidha, imeelezwa kuwa uelewa wa wananchi juu ya masuala ya sheria mkoani Simiyu umeongezeka kwa asilimia 66 kwa kipindi hiki ambapo kwa mwaka 2016 ilikuwa asilimia 10 kabla ya kuanza kwa mradi wa upatikanaji endelevu wa msaada wa kisheria.

 

Hayo yamebainishwa Agosti 7, 2020 na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa shirika la KASODEFO, John Titus, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo na kuongeza kuwa lengo kuu la shirika hilo ni kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi wote wanaotembelea banda lao.

 

Titus amefafanua kuwa kazi kubwa wanayoifanya ni kutoa usaidizi wa kisheria na kwamba wanao wasaidizi wa kisheria 119 ambao waliosajiliwa na kupata mafunzo maalumu kwa ajili ya kutoa elimu na msaada wa kisheria, huku akieleza kuridhishwa na mwitikio wa wananchi juu ya usaidizi wa kisheria unaoendelea kutolewa na shirika hilo.

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka shirika la KASODEFO, John Titus, akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nyakabidi wilayani Bariadi, Simiyu.

“Ongezeko hilo la uelewa limesaidia kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili kwenye vyombo husika, tunawasaidia wakulima na wafugaji kuepuka migogoro ya ardhi baina yao,” amesema Titus.

 

Lila Masuke ni mmoja wa wanufaika wa elimu iliyotolewa kwenye banda la shirika la KASODEFO; amesema amejifunza namna ya kukabiliana na migogoro, ukatili  na matatizo ya ndoa ikiwa ni pamoja na na kujua wapi pa kutoa taarifa ili kupata usaidizi wa kisheria.

 

Naye mkazi wa Bariadi, Lameck Masule, amesema wapo baadhi ya wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili lakini wamekuwa wakiona aibu kujitokeza kupata usaidizi wa kisheria jambo ambalo amesema ni hatari kwao kiafya, maana wengi wao huathirika kisaikolojia na kuishia kuwa walevi kupindukia.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages