NEWS

Tuesday 21 May 2024

Zakayo Wangwe afunguka kufukuzwa kazi Halmashauri ya Tarime VijijiniZakayo Chacha Wangwe
---------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
---------------------------


Zakayo Chacha Wangwe, mtoto wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, Chacha Zakayo Wangwe, ameuita uamzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kumfuta kazi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) kuwa ni ‘uonevu’.

Aidha, Wangwe amedai kosa lililotumika kumfukuza kazi ni la uongo na halina mashiko.

“Kosa lenyewe eti ni utoro, kwanza ni uongo, nilitoa taarifa kuwa naumwa na pia kulikuwa na tatizo la kiusalama na niliripoti polisi. Lakini pia hili ni kosa la kwanza, mtumishi akipatikana na kosa la kwanza anapewa onyo,” Wangwe ambaye pia amewahi kuwa Diwani wa Kata Turwa kuptia CHADEMA katika Jimbo la Tarime Mjini aliiambia Mara Online News mjini Tarime juzi.

Wangwe aliachia udiwania mwaka 2018 na kujiunga na chama tawala - CCM, baadaye akaajiriwa kuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarme (Vijijini).

Ijumaa iliyopita, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lilitangaza kumfukuza kazi Wangwe na watumishi wengine wawili.

Wangwe alisema atakata rufaa didhi ya uamuzi huo wa kumfukuza kazi.

“Nasikitika sana, nitakata rufaa na sababu za kukata rufaa ninazo nyingi. Sijaiba eti ni utoro,” alilalamika Wangwe ambaye hadi anafutwa kazi alikuwa VEO wa kijiji cha Keroti.

Alidai kuwa halmashauri hiyo ilianza kumwadhibu mwaka mmoja uliopita kwa kusimamisha mshahara wake.

“Walianza kuniadhibu kwa kusimamisha mshahara wangu kinyume na utaratibu lakini juzi wanakuja kutangaza kunifukuza kazi,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages