NEWS

Thursday 23 May 2024

DC Tarime atembelea familia za vijana waliopoteza maisha Nyamongo, aonya wavamizi mgodi wa North Mara, apiga marufuku siasa misibaniMkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Maulid Surumbu (katikati mwenye suti) akifariji ndugu wa mmoja wa vijana wawili waliopoteza maisha Nyamongo.
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News, Tarime
-----------------------------------


Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Kanali Maulid Surumbu, leo Alhamisi amekwenda kufariji ndugu wa vijana wawili wa familia tofauti, waliopoteza maisha katika eneo la Nyamongo wakati wakikabiliana na askari polisi.

Vijana hao ni Babu Christopher Iroga, mkazi wa kijiji cha Mjini Kati, na July Mohali, mkazi wa kijiji cha Nyangoto.

Inadaiwa walifikwa na mauti jana jioni wakati wakishirikiana na wenzao kadhaa kukabiliana na askari polisi waliokuwa wakiwazuia kuvamia na kupora mawe ya dhahabu katika mgodi wa North Mara.

Katika safari hiyo, Kanali Surumbu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, amefuatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simion Kiles, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko na wajumbe wa kamati hiyo.


GM Lyambiko (kulia mbele) 
akijumuika na wengine kikaoni.
----------------------------------------------

Kanali Surumbu amesema serikali ya wilaya itagharimia majeneza na chakula katika misiba hiyo.

Ametumia nafasi hiyo pia kupiga marufuku tabia ya wanasiasa wanaotumia matukio ya vifo vya wavamizi wa mgodi wa North Mara ili kujipatia umaarufu kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Misiba yote isitumike kama majukwaa ya siasa, hii ni kwa vyama vyote vya kisiasa vilivyoko wilayani Tarime, haviruhusiwi kufanya siasa kwenye misiba… tufanye siasa zetu kwenye mikutano na siyo kwenye misiba,” amesisitiza Kanali Surumbu.

Aidha, ameelekeza vitongoji vyote katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara kuwa na vitabu vya kutunza kumbukumbu za wakazi wote, huku akisisitiza wananchi kufuata sheria na kuacha vitendo vya kuvamia mgodi huo.

“Wananchi mfuate sheria, kama kuna eneo hamruhusiwi kuingia basi msiingie, kwa sababu mgodi wa North Mara upo kisheria na kuna mikataba kati ya wananchi na mgodi na inatekelezwa,” amesema.

Mapema, Kanali Surumbu (pichani aliyesimama) na msafara wake wamefanya kikao cha dharura na Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) inayoundwa na vijiji 11 vilivyo jirani mgodi wa North Mara kutafuta mbinu za kukomesha vitendo vya uvamizi mgodini.


Sehemu ya viongozi na wajumbe wa CDC wakimsikiliza Kanali Surumbu kwa makini katika kikao hicho.
-----------------------------------------------
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick Gold, kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages