NEWS

Friday 28 August 2020

Mtaalamu ataja kiboko cha magonjwa ya mlipuko

Mtaalamu wa Magonjwa ya Mlipuko, Dkt Khamis Kulemba akitoa mada katika mafunzo hayo kwa wanahabari mkoani Simiyu

MTAALAMU wa magonjwa ya mlipuko kutoka mkoa wa Simiyu, Dkt Khamis Kulemba, amesema jamii ikiwa na utamaduni wa kunawa mikono mara nyingi iwezavyo, magonjwa ya mlipuko yatabaki kuwa historia.

 

Dkt Kulemba amefafanua kuwa magonjwa mengi ya mlipuko yanatokana na tabia za watu ikiwemo kutokuzingatia usafi na kanuni za kiafya ikiwemo kutopenda kunawa mikono mara kwa mara.

 

Ameyasema mwanzoni mwa wiki hii wakati akitoa mada kwa waandishi wa habari kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko, katika mafunzo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Simiyu (SMPC) kwa ufadhili wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Baadhi ya waandishi wa habari wanachama wa SMPC waliohudhuria mafunzo hayo

 

Amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa elimu waliyoipata kwenye mafunzo haypo inaifikia jamii ili kusaidia kuepuka magonjwa, hususan ya mlipuko.

 

"Mfano magonjwa ya kuhara, kuhara damu, kipindupindu, mafua makali na homa ya mapafu kwa asilimia kubwa yanaambukizwa kwa njia ya hewa na kugusana, hivyo  kwa kuzingatia kanuni za afya, haya yanaepukika," amesema Dkt Kulemba. 

Afisa Habari Mkuu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Sara Kibonde, akiwasilisha mada katika mafunzo hayo

 

Naye mmoja wa watoa mada ambaye pia ni Afisa Habari Mkuu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Sara Kibonde, amesema ni muhimu kwa waandishi wa habari kuzingatia na kufuata misingi, maadili, kanuni na taratibu za kitaaluma ili wanachokitoa kwa jamii kiwe na mchango mkubwa, huku akiwasisitiza kujiendeleza kielimu kama sheria inavyotaka.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC), Frank Kasamwa, akizungumza katika mafunzo hayo


Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa SMPC, Frank Kasamwa, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanahabari kujua namna bora ya kuepuka magonjwa ya mlipuko, lakini pia kufikisha elimu waliyoipata kwa jamii.


Nayee mmoja wa mwandishi wa habari, Bahati Sonda ambaye ni mwakilishi wa gazeti la Majira mkoani Simiyu, amesema amepata uelewa wa kutosha kupitia mafunzo hayo na kuahidi kutumia kalamu yake katika kuielimisha jamii umuhimu wa kuzingatia usafi ukiwamo wa kunawa mikono mara kwa mara.

 

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages